IQNA

Mazungumzo ya Obama na Allen kufuatia kuongezeka maandamano yanayotokana na uchomaji moto Qur'ani

12:10 - February 28, 2012
Habari ID: 2282395
Rais Barack Obama wa Marekani amefanya mazungumzo ya simu na John Allen, kamanda wa askari jeshi wa Marekani nchini Afghanistan baada ya kuongezeka maandamano na ghasia zinazotokana na kitendo cha Wamarekani kuchoma moto kitabu kitakatifu cha Qur'ani katika kambi yao ya kijeshi huko Bagram, Afghanistan.
Rais Obama pia amesikitishwa na kitendo cha kuuawa maafisa wawili wa Marekani nchini Afghanistan na kumshukuru Rais Hamid Karzai kwa kuwaomba Waafghani wawe watulivu katika kipindi hiki nyeti. Amedai serikali yake ingali inaheshimu ahadi ilizotoa kwa serikali na wananchi wa Afghanistan na kwamba itaendelea kufanya juhudi za kupambana na magaidi wa mtandao wa al-Qaida na kuiimarisha nchi hiyo ya Asia.
Licha ya kupita siku saba tokea wanajeshi wa Marekani wachome moto kitabu kitakatifu cha Qur'ani, lakini bado maandamano na malalamiko yanaendelea kushuhudiwa katika miji tofauti ya Afghanistan na wala ombi la msamaha lililotolewa na Rais Obama na John Allen kamanda wa askari wa Marekani kwa wananchi wa Afghanistan kuhusiana na suala hilo halijatuliza malalamiko hayo.
Kufuatia kuuawa kwa maafisa wawili wa Marekani nchini Afghanistan, Nato na serikali ya Uingereza zimewaondoa maafisa wao katika wizara kadhaa za nchi hiyo. 961932
captcha