Muhammad Asadi Muwahhed, Mwambata wa Masuala ya Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Zimbabwe amesema kwamba woga na hofu ya Masalafi kuhusiana na kufahamishwa Waislamu fikra na mafundisho ya Ahlul Beit, yaani Watu wa Nyumba ya Mtume (as), inakumbusha hofu waliyokuwa nayo makafiri wa Makka mwanzoni mwa Uislamu kuhusiana na wakazi wa mji huo kusikiliza maneno na ujumbe wa wahyi wa Mtume Mtukufu (saw).
Akizungumza mwishoni mwa mashindano ya hifdhi na kiraa ya Qur'ani Tukufu yaliyoandaliwa siku ya Jumapili na Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya mjini Harare Zimbabwe, kwa lengo la kuwafahamisha vijana wa nchi hiyo shughuli za Qur'ani nchini Iran, Muwahhed amezungumzia umuhimu na nafasi ya Qur'ani Tukufu katika jamii mwanadamu kwa mtazamo wa Ahlul Beit (as).
Sherehe za kufunga mashindano hayo yaliyowashirikisha makarii na mahafidh 20 wa Qur'ani Tukufu nchini Zimbabwe zimehudhuriwa na shakhsia pamoja na wakuu wa taasisi za Kiislamu za nchi hiyo.
Akizungumzia umuhimu wa Qur'ani katika jamii ya Waislamu, Muwahhed amesema dini ya Kiislamu ina desturi na sheria nyingi ambazo zimesimama juu ya msingi wa Qur'ani kwa manufaa ya jamii nzima ya mwanadamu. Amegusia tabia ya baadhi ya makundi ya Kisalafi yaliyo na woga na hofu kubwa juu ya ujumbe wa Ahlul Beit wa Mtume (saw) kuwafikia Waislamu na kusema kuwa mwanazoni mwa kutangazwa ujumbe wa Mtume Mtukufu (saw) Makafiri wa Kureishi walikuwa na wasiwasi na hofu kubwa kuhusu watu kusikia na kupata kujua ukweli wa mambo kuhusiana na ujumbe huo wa wahyi.
Amesema licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na makafiri za kuzuia ujumbe huo kuwafikia watu, lakini wengi wa watu hao na jamaa zao walipata kusikia na kuvutiwa na ujumbe huo uliposomwa na Mtume (saw) kupitia aya za Qur'ani Tukufu. Wengi wa watu walimsikia Mtume akisoma aya za Qur'ani na kisha kurejea makwao na kuwafahamisha jamaa zao maneno ya mvuto mkubwa na ya kushangaza yaliyotamkwa na Mtume Mtukufu (saw). Amesema watawala dhalimu wa zama hizo kamwe hawakuridhishwa na hali hiyo na kwa hivyo walifanya kila waliloweza ili kuvuruga juhudi za Mtume za kusambaza mafundisho ya dini ya Mwenyezi Mungu katika jamii, lakini kwamba juhudi zao hizo ziligonga mwamba na mwishowe tawala zao kusambaratika.
Mwambata huyo wa Kiutamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Zimbabwe amekumbusha kwamba siri ya ushindi, ukakamavu na uthabiti wa mfumo wa Kiislamu wa Iran mbele ya njama zote zinazotekelezwa na maadui hii leo inatokana na kushikama kikamilifu mfumo huu na mafundisho ya Qur'ani Tukufu. Amesisitiza kwamba madamu mfumo huu utaendelea kuwa na msimamo huohuo, hautapatwa na madhara yoyote ya maadui. 1002843