IQNA

Iran yakabidhiwa uenyekiti wa mkutano wa mawaziri wa nje wa NAM

20:14 - August 28, 2012
Habari ID: 2400911
Mepema leo Misri umekabidhi uenyekiti wa vikao vya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama katika Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Ramzi Izzuddin Ramzi leo mwanzoni mwa mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa NAM mjini Tehran, ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa maandalizi mazuri ya mkutano wa sasa wa jumuiya hiyo na kumkabidhi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Akbar Salehi uenyekiti wa vikao vya mkutano huo.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameishukuru Misri kwa juhudi zake za kipindi cha miaka mitatu iliyopita katika jumuiya ya NAM na kusema hati ya mkutano wa sasa wa Tehran inapasa kudhamini maslahi ya nchi zote wanachama. Salehi amesema changamoto za dunia ya sasa ni tata na ngumu zaidi kuliko zile za kipindi cha vita baridi na kusisitiza kuwa, hii leo dunia inakabiliwa na changamoto kubwa zinazotokana na utandawazi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa masuala ya ustawi endelevu yanapaswa kupewa umuhimu mkubwa zaidi na kuongeza kuwa, fursa hii inapaswa kutumiwa kwa ajili ya kusisitiza juu ya masuala yanayozikutanisha pamoja nchi wanachama wa NAM.
Wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, kufanyika kwa mkutano wa 16 wa jumuiya ya Nam mjini Tehran na kukabidhiwa uenyekiti wa jumuiya hiyo kwa Iran ni fursa isiyokuwa na kifani kwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote ya kubuni sera na siasa mpya kwa ajili ya mustakbali bora katika kipindi hiki muhimu cha historia. Mkutano wa sasa wa Tehran unatajwa kuwa ndio muhimu zaidi wa jumuiya ya NAM katika kipindi chote cha uhai wake wa nzaidi ya miaka 50 na kwa msingi huo inatarajiwa kuwa nchi wanachama zitatambua umuhimu mkubwa wa kipindi cha sasa na kuielekeza jumuiya hiyo kubwa ya kimataifa upande wa kuwa na taathira kubwa zaidi katika masuala ya kimataifa. Vilevile hapana shaka kuwa, katika kipindi cha uenyekiti wake wa miaka mitatu ijayo kwenye jumuiya ya NAM, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itafanya jitihada kubwa kuhakikisha kwamba, NAM inaimarishwa zaidi na kuwa na nafasi muhimu katika maamuzi ya kimataifa.
Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote ambayo ina wanachama 120 ndiyo jumuiya kubwa zaidi ya kimataifa baada ya Umoja wa Mataifa. Kwa mtazamo huo mkutano wa 16 wa jumuiya hiyo hapa mjini Tehran ambao umepewa anwani ya: "Amani Endelevu katika Kivuli cha Uongozi wa Pamoja wa Dunia", unaweza – katika kipindi muhimu cha sasa- kupiga hatua kubwa katika utekelezaji wa malengo ya NAM. Malengo hayo ni pamoja na kupinga ubeberu na dhulma katika mahusiano ya kimataifa, ustawi endelevu na kutumia vyema fursa za kiuchumi na kukabiliana na vitisho vya kiusalama na silaha za nyuklia. Malengo mengine muhimu yanayopewa kipaumbele na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya jumuiya hiyo ni kufanya juhudi za kuondoa ubaguzi, kuheshimiwa haki za mataifa mbalimbali hususan taifa linaloendelea kukandamizwa la Palestina, kuleta mlingano katika ugavi wa mamlaka kati ya asasi za Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kushirikishwa na kupewa nafasi muhimu jumuiya ya NAM katika Baraza la Usalama.
Masuala hayo yote yamesisitizwa leo katika hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika ufunguzi wa mkutano wa Mawaziri wa Nje wa nchi wanachama katika Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote. 1086837



captcha