Ameweka wazi sababu za kinyongo cha Wazayuni dhidi ya Uislamu na Qur’ani na akasisitiza kuwa, kama wanasiasa wa Marekani wanasema kweli katika madai yao kwamba hawakuhusika katika jinai hii, basi wanapaswa kuwapa adhabu inayonasibiana na jinai hii wale wote waliohusika na uhalifu huo mkubwa na waliowasaidia kifedha ambao wamezitia simanzi na maumivu nyoyo za mataifa ya Waislamu.
Matini kamili ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu
Mwenyezi Mungu Muweza na Hakimu amesema: “Wanataka kuzima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa midomo yao na Mwenyezi Mungu atatimiza nuru yake japokuwa makafiri wanachukia.”
Taifa azizi la Iran, umma wa mkubwa wa Kiislamu.
Kwa mara nyingine tena mkono muovu wa maadui wa Uislamu umeweka wazi kinyongo na uhasama wake mkubwa kwa kumvunjia heshima Mtume Mtukufu (saw) na kudhihirisha hasira za majmui khabithi ya Wazayuni dhidi ya kung’ara kunakoongezeka kila siku kwa Uislamu na Qur’ani katika dunia ya sasa kwa hatua hiyo ya kiwendawazimu na ya kueneza chuki.
Inatosha katika maovu ya watenda jinai hii na dhambi zao kubwa kwamba, wamelenga sura takatifu na inayong’ana zaidi ya watukufu wa ulimwengu kwa mawimbi ya upuuzi wao unaotia kinyaa. Siasa za kihasama za Wazayuni, Marekani na vinara wengine wa ubeberu wa kimataifa ndizo zilizohusika na harakati hiyo iliyojaa shari na kwa dhana zao batili, wanataka kuporomosha na kudunisha matukufu ya Kiislamu mbele ya macho ya vizazi vya vijana katika ulimwengu wa Kiislamu na kuzima hisia zao za kidini.
Lau kama wasingeunga mkono sehemu za kwanza za mnyororo huu muovu yaani Salman Rushdie, mchora vikatuni wa Denmark na makasisi wa Kimarekani waliochoma moto Qur’ani, na kuacha kuagiza makumi ya filamu zinazopiga vita Uislamu kutoka kwenye makampuni ya wawekezaji wa Kizayuni, basi hali isingefikia kiwango hiki cha kutenda dhambi kubwa na isiyosameheka.
Mtuhumiwa wa kwanza katika jinai hii ni Wazayuni na serikali ya Marekani. Kama wanasiasa wa Marekani wanasema kweli katika madai yao kwamba hawakuhusika na uhalifu huo, basi wanapaswa kuwapa adhabu inayonasibiana na jinai hii wale wote waliohusika na uhalifu huo mkubwa na waliowasaidia kifedha ambao wamezitia simanzi na maumivu nyoyo za mataifa ya Waislamu.
Ndugu Waislamu kote duniani pia wanapaswa kuelewa kwamba, harakati hizi zilizofeli za maadui dhidi ya mwamko wa Kiislamu ni kielelezo cha adhama na umuhimu wa mwamko huo na bishara ya kustawi kwake zaidi. Mwenyezi Mungu atashinda kwa jambo lake.
Sayyid Ali Khamenei
23 Shahrivar 1391 (13 Septemba 2012)
1097628