
Huku akielezea kufurahishwa kwake na kuzaa matunda muqawama
wa taifa la Iran mbele ya vikwazo vya kidhulma na kurudi nyuma pande zilizokuwa
zinakabiliana na Iran kutokana na jitihada za wasomi na wanasayansi wa nyuklia
wa Iran na jitihada za watu wote waliohusika kwenye mazungumzo hayo,
amemsisitizia nukta tano muhimu Rais Hassan Rouhani.
Matini kamili ya majibu hayo ni kama ifuatavyo:
Bismillahir Rahmanir Rahim
Janab Dk. Rouhani,
Mheshimiwa Rais (wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran)
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh
Ninaitumia fursa hii kuelezea furaha yangu kwa kuona kuwa muqawama wa taifa
kubwa la Iran mbele ya vikwazo vya kidhulma na jitihada za wataalamu wetu wa
nyuklia katika kuendeleza teknolojia hiyo muhimu na juhudi zisizochoka za timu
za mazungumzo, hatimaye zimepelekea pande za upande wa pili ambazo baadhi yake
ni maarufu kwa kulifanyia uadui taifa la Iran, zimelazimika kurudi nyuma na
kuondoa baadhi ya vikwazo hivyo vya kibeberu; na ninakushukuru wewe na timu nzima
ya mazungumzo na mheshimiwa waziri mwenyewe (wa mambo ya nje wa Iran) na
wahusika wote. Ninapenda kuitumia fursa hii kukumbusha masuala yafuatayo:
Mosi: Ihakikishwe kuwa upande wa pili unatekeleza kikamilifu ahadi zake. Hata
hivyo matamshi ya siku mbili tatu zilizopita yaliyotolewa na baadhi ya
wanasiasa wa Marekani yanatufanya tuwe na mtazamo mbaya kikamilifu.
Pili: Maafisa wote wa serikali watahadharishwe kwamba, utatuzi wa matatizo ya
kiuchumi nchini yamo katika jitihada zisizosita na za hekima za sekta zote
nchini kupitia uchumi wa kimuqawama na kwamba kuondolewa vikwazo tu hakutoshi
katika kuleta ustawi wa kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Tatu: Katika kulitangaza suala hilo inabidi lipewe umuhimu suala la
kuwatangazia wananchi kuwa, taifa limegharamika mno katika kufikia
kilichofikiwa kwenye jambo hili. Maandishi na matamshi yanayotolewa kwa lengo
la kujaribu kufifiliza na kupunguza umuhimu wa uhakika huo na kuona kuwa jambo
hili limewezekana kutokana na kufadhiliwa na upande wa Magharibi, kwa hakika
hayawatendei haki wananchi.
Nne: Haya matunda yaliyopatikana mbele ya kambi ya kiistkbari na kibeberu
katika suala hili, yamepatikana kutokana na muqawama na kusimama kidete taifa.
Jambo hili linapaswa liwe funzo kubwa kwetu sote katika masuala na mambo yote
yanayohusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Tano: Kwa mara nyingine ninasisitiza kwamba isije ikasahauliwa tabia ya tawala
za kibeberu hususan Marekani ya hadaa na kuvunja ahadi katika suala hili na
masuala mengineyo.
Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akupe taufiki wewe na viongozi wengine
nchini.
Sayyid Ali Khamenei
29 Dei 94
(Januari 19, 2016).