
Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi jana Jumatano liiliiweka harakati ya Muqawama ya Hizbullah na makundi yote yenye mfungamano na harakati hiyo kwenye orodha eti ya waungaji mkono ugaidi, kwa lengo la kuishinikiza zaidi harakati hiyo ambayo ina nafasi kuu katika matukio ya ndani ya Lebanon na ambayo inaendesha mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni na vile vile ikiwa na nafasi muhimu katika kutatua mgogoro wa Syria.
Nchi za kusini mwa Ghuba ya Uajemi mwaka 2013 pia ziliwawekea vikwazo baadhi ya wanachama wa Hizbullah kufuatia kuweko kijeshi Hizbullah katika mgogoro wa Syria. Aidha mwaka huo huo baadhi ya nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ikiwemo Saudi Arabia, Imarati na Bahrain ziliitaja harakati ya Hizbullah ya Lebanon kuwa ni kundi la kigaidi.
Wakati huo huo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa hatua ya kuiweka harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika orodha ya makundi ya kigaidi ni sawa na kufumbia macho jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel suala ambalo halina faida kwa usalama na amani na eneo la Mashariki ya Kati.
Hossein Amir-Abdollahian ambaye alikuwa akijibu hatua ya Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi ya kuiweka Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi amesema kuwa, wale wanaoiita Hizbullah kuwa ni magaidi wanahujumu usalama na amani ya Lebanion kwa kutaka au bila ya kutaka. Amir-Abdollahian ameongeza kuwa, Iran inajifakharisha kwa Hizbullah ambayo ni mstari wa mbele wa mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kinara wa mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa umoja wa kitaifa, usalama na amani ya Lebanon na kuunga mkono mshikamano wa makundi yote ya Lebanon ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele katika siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
3480057