IQNA

Siku ya Kimataifa ya Kuonyesha Mshikamano na Taifa la Palestina

15:22 - December 01, 2019
Habari ID: 3472246
TEHRAN (IQNA) - Tarehe 29 Novemba iliadhimishwa kote duniani kama Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Taifa la Palestina

Mwaka 1977 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza Tarehe 29 Novemba kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Taifa la Palestina. Sababu ya hatua huyo ya Umoja wa Mataifa ni nafasi na mchango wa Baraza Kuu la umoja huo katika kuigawa ardhi ya Palestina. Tarehe 29 Novemba 1947 baraza hilo lilipasisha azimio nambari 181 lililoidhinisha kugawanywa ardhi ya Palestina. Kwa mujibu wa azimio hilo Palestina iligawanywa sehemu mbili kwa ajili ya kuundwa dola la Kiyahudi na nchi ya Palestina. Pamoja na hayo hadi sasa utawala ghasibu wa Israel haujawahi kuheshimu azimio hilo na daima umekuwa ukijitanua na kutwaa ardhi zaidi za Palestina kwa kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi iliyoghusubiwa. Tabia hiyo ya Israel ya kutoheshimu azimio nambari 181 ilikuwa sababu ya Baraza Kuu kuchukua uamuzi wa kuitangaza tarehe 29 Novemba kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Taifa la Palestina ili angalau iwapoze Wapalestina kwa njia moja au nyingine. Hata hivyo tunaweza kusema kuwa, kutangazwa siku hiyo hakujawa na taathira yoyote katika hali ya Palestina licha ya kupita miaka 42 sasa. 

Wapalestina wananyimwa haki za binadamu

Kwa sasa Wapalestina wananyimwa haki zao za kimsingi kabisa za binadamu. Zaidi ya Wapalestina milioni tano wanaishi ukimbizini na maelfu miongoni mwao hawana makazi kabisa. Eneo la Ukanda wa Gaza limekuwa chini ya mzingiro wa pande zote tangu mwaka 2006, Wapalestina zaidi ya 5,700 wamefungwa katika jela za Israel na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina unaendelea kwa kasi kubwa.

Kumetajwa sababu nyingi za kutokuwa na taathira hatua ya Baraza Kuu la UN ya kuitangaza tarehe 29 Novemba kuwa Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano wa Taifa la Palestina. Miongoni mwa sababu muhimu ni kwamba dhati na asili ya utawala wa Israel ni ugaidi, uvamizi na ukatili. Utawala huo ambao ulivamia na kutwaa ardhi ya Palestina kwa msaada wa nchi za Magharibi, unakutambua kuzikaliwa kwa mabavu ardhi hizo kuwa moja ya sera zake muhimu.

Sababu ya pili ni kwamba, utawala huo ghasibu unakingiwa kifua na kupewa himaya na nchi kubwa hususan Marekani na nchi hizo zinapuuza na kufumbia macho uhalifu na jinai zote zinazofanywa na Israel bali pia zinatayarisha mazingira ya kudumishwa jinai hizo.

Israel inakiuka maazimio ya Baraza la Usalama

Sababu ya tatu ni kwamba, maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa si lazima kutekelezwa, na kimsingi huwa ni hatua ya kinembo tu. Kwa msingi huo utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unakiuka maazimio muhimu na ya lazima kutekezwa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hausiti hata kidogo kukanyaga maazimio la Baraza Kuu.

Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, hatua ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ya kuitangaza tarehe 29 Novemba kuwa Siku ya Kimataifa ya Konesha Mshikamano na Taifa la Palestina haikuwa na faida za kivitendo kwa watu wa Palestina na zaidi inakumbusha jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taifa hilo.     

3860312

captcha