IQNA

ICJ yasikiliza kesi kuhusu mauaji ya kimbari ya Waislamu nchini Myanmar

18:09 - December 10, 2019
Habari ID: 3472265
TEHRAN (IQNA) Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) imeanza kusikiliza kesi kuhusu mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Myanmar kufuatia shtaka ambalo limewasilishwa na Gambia.

Kesi hiyo, ambayo imeanza leo Jumanne huko The Hague,  ni hatua ya kwanza ya kisheria ya kuwafikisha kizimbani watawala wa Myanmar ambao wamehusika na jinai dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Gambia, ambayo imewasilisha kesi hiyo kwa niaba ya nchi 57 wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), imetoa wito kwa ICJ kuchukua hatua za dharura kusitisha vitendo vya Myanmar vya mauaji ya kimbari dhidi ya Warohingya.

Akizungumza katika cha mahakama, Waziri wa Sheria wa Gambia Abubacarr Tambadou amesema: "Kile ambacho Gambia inauliza ni kuwa, muitake Myanmar isitishe mauaji na ukatili ambao unaendelea na isiamamis mauaji ya kimbari dhidi ya watu wake."

Mwezi uliopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema bado anaendelea kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Myanmar, ikiwemo katika jimbo la Rakhine kutokana na kukandamizwa Waislamu wa jamii ya Rohingya katika eneo hilo.

Ikumbukwe kuwa, Agosti 25 mwaka 2017 Waislamu wapatao 740,000 wa jamii ya Rohingya walilazimika kuyahama makazi yao kwa umati katika jimbo lao la Rakhine na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh walikojiunga na wenzao wengine laki mbili waliokuweko nchini humo, baada ya vikosi vya jeshi la Myanmar na Mabudhha wenye misimamo ya kufurutu ada kuanzisha wimbi kubwa la hujuma na ukandamizaji dhidi ya Waislamu hao.

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein aliesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Wakati huo huo,  Hla Kyaw, Mwenyekiti wa Baraza la Ulaya la Jamii ya Rohingya ameelezea matumaini yake kuwa kesi iliyofikishwa ICJ itakuwa mwanza wa haki na uwajibikaji kufuatia miongo kadhaa ya masaibu ya jamii ya Rohingya nchini Myanmar.

Amesema Waislamu wa jamii ya Rohingya wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kupata haki na sasa wana matumaini kuwa mchakato wa ICJ utakuwa wa haraka.

3470075

captcha