IQNA

Misikiti Marekani yafungua milango kwa wasiokuwa Waislamu

15:54 - December 11, 2019
Habari ID: 3472269
TEHRAN (IQNA) – Misikiti katika jimbo la Ohio nchini Marekani imetanga siku maalumu ambapo wasiokuwa Waislamu wamekaribishwa ili kupata kuufahamu Uislamu zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa, Waislamu katika jimbo la Ohio nchini Marekani wamefanya hafla ya siku moja iliyopewa jina la "Milango Wazi" katika misikiti yao kwa kuwakaribisha wasio Waislamu misikitini humo ili waweze kuuelewa Uislamu.

Hafla hiyo ya "Milango Wazi" katika misikiti ya jimbo la Ohio imehudhuriwa na wafuasi wa dini mbalimbali, lengo likiwa ni kuhamasisha kuwepo uhusiano imara baina ya jamii mbali mbali na kuwalingania watu mafunzo ya dini tukufu ya Kiislamu.

Hafla ya aina hiyo ilifanyika kwa mara ya kwanza mwaka uliopita wa 2018 katika jimbo hilo hilo la Ohio; na Jumapili pia misikiti kadhaa ya jimbo hilo ilikuwa wenyeji wa kuwapokea watu mbali mbali wasio Waislamu.

Luby Abdurrahman, mmoja wa wanachama wa jumuiya ya Rahmat Dayton, iliyoko katika mji wa Miamisburg jimboni Ohio, ambayo ndiyo iliyoendesha hafla hiyo katika msikiti wa mji huo amesema: Programu hiyo imefanyika kwa mara ya kwanza katika mji huo na imepokelewa vizuri na watu.

Licha ya hujuma, mashambulio na unyanyasaji mkubwa unaofanywa na makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka ya mrengo wa kulia na ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Waislamu nchini Marekani, jumuiya na asasi mbali mbali za Kiislamu za nchi hiyo zinaendelea kufanya shughuli za tablighi ya dini hiyo tukufu.

Rais wa Marekani Donald Trump, mbali na kunyamazia kimya kila mara vitendo vya hujuma na ukatili vinavyofanywa na makundi ya ubaguzi na ya mrengo wa kulia, baadhi ya wakati amekuwa hata kwa namna fulani akiyaunga mkono makundi hayo. Tokea Trump aingie madarakani kumeshuhudiwa ongezko kubwa la vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na kwa msingi huo Waislamu nchini humo wameanzisha kampeni mbali mbali za kuelimisha umma Marekani kuhusu Uislamu ili kuondoa taswira ghalati inayoenezwa na vyombo vya habari na wanasiasa.

Waislamu katika maeneo mengi duniani sasa wameanzisha "Siku ya Milango Wazi" katika misikiti ili kuwaelimisha wasiokuwa Waislamu katika jamii zao kuhusu Uislamu.

/3862790

captcha