IQNA

Bunge la India lapitisha sheria yenye kuwabagua Waislamu

9:30 - December 12, 2019
Habari ID: 3472272
TEHRAN (IQNA) – Bunge la Seneti nchini India limepitisha muswada wa sheria ambayo inawapa uraia wahajiri kutoka Pakistan, Bangladesh na Afghanistan lakini kwa sharti kuwa wasiwe Waislamu.

Sheria hiyo inalenga kuwapa uraia wa India Mabuddha, Wakristo, Wahindu, Wajain, Waparsis na Wakalasinga ambao waliondoka katika nchi hizo tatu kabla yam waka 2015.

Bunge la Seneti la India (Rajya Sabha) lilipasisha muswada huo wa sheria Jumatano na sasa rais wa nchi hiyo anatazamiwa kuitia saini ili jiwe sharia rasmi.

Muswada huo wa sheria uliwasilishwa bungeni na serikali yenye misimamo mikali ya Kihindu ya Waziri Mkuu Narendra Modi ambaye amepongeza upasishwaji sheria hiyo.

Wabunge wa upinzani wamepinga muswada huo na kusema watafika mahakamani kuupinga. "Leo ni siku mbaya katika historia ya katiba ya India," amesema Sonia Gandhi wa chama kikuu cha upinzani cha Congress. Wataalamu wanasema muswada huo unakiuka katiba kwani unataja dini kuwa msingi wa uraia na hiyo kuwabagua Waislamu milioni 200.

Hayo yanajiri wakati ambao mwezi Agosti, serikali ya India ililipokonya eneo linalozozaniwa lenye Waislamu wengi la Jammu na Kashmir hadhi maalumu ya kujitawala kwa lengo la kulidhibiti zaidi.

Mwezi uliopita pia, katika hukumu ya uonevu na upendeleo wa wazi iliyotolewa kwa manufaa ya Wahindu wenye misimamo ya chuki na kufurutu mpaka, Mahakama ya Juu Kabisa ya India imeamua kuwapatia Wahindu eneo walipoubomoa msikiti wa kihistoria wa Babri ili wajenge hekalu lao la Ram.

Wakosoaji wanasema kama lengo la serikali ya India ni kuwasaidia watu wanaokandamizwa katika nchi jirani, basi ingewapa uraia pia Waislamu wa jamii ya Rohingya ambao wanakabiliwa na mauaji ya kimbari nchini jirani ya Myanmar.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na maafisa wengine wa chama chake tawala cha chenye misimamo mikali ya Kihindu BJP, wamekuwa wakitekeleza sera za kuwakandamiza Waislamu nchini humo.

3863558

captcha