IQNA

Waislamu waanza kuondoka Uingereza baada ya Johnson kuchaguliwa

13:28 - December 16, 2019
Habari ID: 3472282
TEHRAN (IQNA) – Baadhi ya Waislamu wa Uingereza wameanza kujitayarisha kuondoka nchini humo wakihofia usalama wao baada ya uchaguzi ambao unamuandalia njia Boris Johnson kuendelea kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kwa muda miaka mitano.

Kati ya waliotangaza wazi azma ya kuondoka Uingereza ni Manzoor Ali, mkuu wa shirika moja la Kiislamu la kutoa misaada la Barakah Food Aid mjini Mancheste ambaye anasema ana hofu kuhusu mustakabali wa watoto. Ameongeza kuwa: "Nahofia usalama wangu, nahofia mustakabali wa watoto wangu."

Hayo yanajiri baada ya Johnson kutuhumiwa kuwa anaeneza chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi kufuatia matamshi tata aliyowahi kutoa huko nyuma hasa mwaka 2005 alipoandika makala na kudai kuwa ni jambo linalotarajiwa kwa umma kuwa na hifu kuhusu Uislamu.

Johnson aidha alikosolewa vikali alipowalinganisha wanawake Waislamu wanaovaa nikabu kuwa ni sawa na 'masanduku ya barua na wezi wa benki' katika makala aliyoandikia gazeti la Telegraph mwaka jana.

Ali anasema shirika lake la msaada limekuwa likiendesha shughuli zake kwa muda wa miaka 10 na huwasaidia watu kutoka tabaka zote za jamii wakiwemo wasiokuwa Waislamu.  Anaongeza kuwa, ingawa yeye ni mwenyeji wa Uingereza na hana sehemu nyingine, ameamua kuhama. Ali, mwenye watoto watatu, anasema anatafakari kuhamia New Zealand kutokana na ukarimu ambao ulionyeshwa na waziri mkuu, Jacinda Ardern, baada ya hujuma dhidi ya misikiti mjini Christchurch ambapo Waislamu 51 waliuawa na gaidi mwenye misimamo ya kuvurutu ada.

Naye Bi. Eidan, 38, mtaalamu wa masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano ambaye huvaa Hijai ni mkazi wa kaskazini mwa London na anasema ana hofu kubwa sana baada ya uchaguzi kwani aliwahi kuvuliwa mtandio wake hadharani huku baadhi wakimuita 'gaidi.' Eidan anasema anatafuta kazi maeneo mengine kama vile Uturuki au Pakistan.

Baraza la Waislamu Uingereza (MCB) linasema kwa muda mrefu Waislamu wamekuwa na wasiwasi kuhusu siasa za Uingereza na chama kinachotawala hivi sasa.

Hayo yanajiri wakato ambao kumefanyika maandamano makubwa yameripotiwa katika maeneo mbali mbali nchini Uingereza kupinga matokeo ya uchaguzi wa bunge ambapo chama cha Kihafhidhina (Conservative) cha Waziri Mkuu Boris Johnson kimepata ushindi.

Maandamano yaliripotiwa katikati mwa jiji la London katika medani ya Trafalgar na pia nje ya makao rasmi ya waziri mkuu katika barabara ya 10 Downing.  Waandamanaji walikuwa wamebaba mabango yaliyoandikwa, "Boris Johnson si waziri mkuu wangu," "Pingeni utawala wa Wahafidhina" na "Wakimbizi Wanakaribishwa". Watu kadhaa wamekamatwa na vikosi vya usalama katika maandamano hayo. Katika uchaguzi wa Bunge la Uingereza uliofanyika Alhamisi iliyopita chama cha Wahafidhina kimepata viti 365 kati ya viti 650 vya Bunge kikifuatiwa na chama cha Leba kinachoongozwa na Jeremy Corbyn kilichopata viti 203.

3470121

captcha