IQNA

Rais Rouhani: Marekani inafuata njia isiyo sahihi kuhusu taifa la Iran

16:46 - January 16, 2020
Habari ID: 3472378
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Marekani inafuata njia isiyo sahihi kuhusu taifa la Iran. Ameongeza kuwa, taifa la Iran limezidi kuwa na nguvu na limekuwa imara zaidi mbele ya njama na vikwazo vya Marekani.

Rais Rouhani amesema hayo leo Alkhamisi katika Kongamano la 59 la Bodi Kuu ya Benki Kuu ya  Iran na huku akitoa mkono wa pole kwa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema, jinai ya Marekani ya kumuua kigaidi kamanda huyo wa kijeshi imeliathiri eneo zima la Asia Magharibi na duniani kote kiasi kwamba Waislamu wote, kuanzia Kashmir hadi Afrika wameelezea kuumizwa mno na jinai hiyo ya Marekani.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile amesema, ni nchi chache sana zenye uthubutu wa kushambulia kwa makombora kambi ya kijeshi ya Marekani akiongeza kuwa, baada ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Soleimani, Iran ya Kiislamu imeshambulia kwa makombora kambi ya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq na kumlazimisha Donald Trump kurudi nyuma na kutothubutu kutekeleza kivitendo vitisho vyake dhidi ya Iran.

Amesema, mipango ya Marekani ni ghalati na mibovu kikamilifu katika eneo hili la Asia Magharibi wakati ambapo taifa la Iran limezidi kuwa na nguvu na limekuwa imara mbele ya njama za Marekani na wenzake.

Rais Rouhani amegusia pia mashinikizo na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na kusema, watu ambao huko nyuma walikuwa wakishirikiana na rais wa Marekani, Donald Trump, hivi sasa wamejitenga na serikali yake na wanakiri kwamba Trump ameiletea matatizo mengi dunia nzima, kuanzia barani Ulaya hadi Mexico.

3872062

captcha