IQNA

Baraza mpya la mawaziri nchini Lebanon, serikali ya mateknokrati

13:11 - January 23, 2020
Habari ID: 3472397
TEHRAN (IQNA)- Hassan Diab Waziri Mkuu Mpya wa Lebanon Jumanne 21 Januari alitangaza rasmi baraza lake la mawaziri.

Moja ya tofauti kuu za baraza la mawaziri la Diab na lile lililotangulia huko Lebanon chini ya uongozi wa Saad Hariri ni hii kuwa baraza jipya la mawaziri la Lebanon linaundwa na mateknokrati 20; wakati baraza la mawaziri la serikali ya Waziri Mkuu Saad Hariri lilikuwa na mawaziri 30. Moja ya matakwa ya wananchi wa Lebanon lilikuwa ni kupunguzwa ukubwa wa serikali na gharama zake. Kwa hiyo kupungua idadi ya mawaziri 10 katika serikali hii mpya ya Lebanon ni wazi kuwa kutapunguza pia gharama na hivyo kudhamini moja ya matakwa ya watu wa nchi hiyo.

Nyuso mpya

Tofauti nyingine ni hii kwamba shakhsia wasio na umashuhuri wanaonekana ndani ya  serikali hii ya Hassan Diab. Moja ya matakwa ya wafanya maandamano wa Lebanon lilikuwa ni kuwaondoa kikamilifu wale wote waliohudumu katika serikali iliyopita. Waziri Mkuu Hassan Diab kivitendo amedhamini takwa hilo la wananchi kwa kuwaarifisha shakhsia wasiojulikana sana nchini humo. Tofauti nyingine kati ya serikali hii mpya na ile ya zamani ya Lebanon ni  kwamba; wanawake 6 wameteuliwa kuhudumu katika serikali  hiyo mpya ambapo kwa mara ya kwanza mwanamama ameteuliwa kuongoza Wizara ya Ulinzi na wakati huo huo kuwa  Naibu Waziri Mkuu.

Kuhitimisha Machafuko

Kipaumbele chenye umuhimu mkubwa cha serikali mpya ya Lebanon ni kuhitimisha machafuko nchini humo. Diab amechukua hatua ya awali ya kutilia maanani matakwa ya wananchi kwa kuunda serikali. Waziri Mkuu wa Lebanon amesema baada ya kuunda serikali hiyo mpya kwamba ataendelea kuchukua hatua nyingine ili kuwadhaminia wananchi matakwa yao na kuhitimisha machafuko nchini humo. Pamoja na hayo yote, serikali mpya ya Lebanon inakabiliwa na changamoto kadhaa muhimu. Changamoto ya kwanza ni kuwa baadhi ya mirengo ndani ya nchi inayoungwa mkono na nchi ajinabi ambayo haijaridhishwa na hatua ya kuarifishwa Diab kuwa Waziri Mkuu Mpya wa Lebanon haitaki kuona machafuko ndani ya Lebanon yanamalizika. Kuhusiana na suala hilo wafanya maandamano pia walimiminika mitaani kuonyesha upinzani wao kwa serikali mpya masaa machache tu baada ya kutangazwa baraza jipya la mawaziri; katika hali ambayo serikali hii mpya imezingatia  na kutoa kipaumbele cha awali kwa matakwa ya wananchi. Kwa msingi huo serikali mpya ya Lebanon inapasa katika hatua yake ya awali, kuandaa mazingira ya kuhitimishwa machafuko; jambo ambalo linaonekana kuwa gumu.

Matatizo ya kimaisha ya wananchi

Changamoto nyingine ni urithi aliourithi Hassan Diab kutoka kwa serikali zilizotangulia khususan serikali ya Saad Hariri. Urithi ulio na umuhimu zaidi ni matatizo ya kimaisha ya wananchi na uchumi ambayo yalikuwa sababu kuu ya kuanza maandamano huko Lebanon Oktoba 17 mwaka jana. Kupungua mishahara na uwezo wa manunuzi wa wafanyakazi na wastaafu, nyongeza ya kodi, kupungua thamani ya sarafu ya nchi hiyo, kupigwa marufuku kuingizwa sarafu ya dola huko Lebanon, kukimbia nchi wawekezaji na wasomi, kuwepo nakisi kubwa ya bajeti, deni kubwa la nje na pia ufisadi uliokita mizizi; zote hizi zinatajwa kuwa changamoto kubwa ambazo zinapasa kufanyiwa kazi na serikali mpya ya Lebanon. Hatua ya kwanza inayopasa kuchukuliwa ili kupunguza matatizo yote haya kwanza ni kuwa, amani na uthabiti vinapasa kuwepo nchini. Pili, wananchi wawe na subira na waipe serikali muda wa kufanya kazi; na tatu, serikali inahitaji kuwa na uwiano na nidhamu sahihi. Nukta ya mwisho ni kwamba kuundwa serikali mpya huko Lebanon katika marhala ya awali ni mafanikio kwa Hassan Diab na katika marhala ya pili pia ni mafanikio kwa rais wa nchi hiyo Michel Aoun na mirengo kama Muungano wa Muqawama ambayo imeshirikiana na Waziri Mkuu mpya katika kuasisi serikali.

3873561

captcha