IQNA

21:13 - January 24, 2020
News ID: 3472401
TEHRAN (IQNA) - Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) imeitaka serikali ya Myanmar kuchukua hatua za dharura za kuzuia mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Rohingya, ikisisitiza kuwa Warohingya hao wamesababishiwa machungu na maumivu yasiyoweza kufutika au kurekebishika.

Akisoma agizo la majaji wote 17 wa mahakama hiyo iliyoko The Hague nchini Uholanzi jana Alkhamisi, Rais wa ICJ, Abdulaqawi Ahmed Yusuf, amesema, "Mynamar imesababisha hasara isiyofidika kwa kukanyaga haki za Warohingya."

Novemba mwaka uliopita, Gambia iliwasilisha faili la kesi ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Warohingya katika mahakama hiyo ya juu ya Umoja wa Mataifa iliyoko The Hague.

Gambia ilisema imechukua hatua hiyo ili kutafuta haki na kuhakikisha wahusika wa mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Myanmar dhidi ya Warohingya katika mkoa wa Rakhine wanabebeshwa dhima.

Faili hilo limeanza kusikilizwa na ICJ katika hali ambayo, wiki chache zilizopita, maafisa wa Umoja wa Mataifa walitoa wito wa kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ili kushughulikia jinai zinazofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine nchini humo.

Ikumbukwe kuwa, Agosti 25 mwaka 2017 Waislamu wapatao 740,000 wa jamii ya Rohingya walilazimika kuyahama makazi yao kwa umati katika jimbo lao la Rakhine na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh walikojiunga na wenzao wengine laki mbili waliokuweko nchini humo, baada ya vikosi vya jeshi la Myanmar na Mabudhha wenye misimamo ya kufurutu ada kuanzisha wimbi kubwa la hujuma na ukandamizaji dhidi ya Waislamu hao.

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein aliesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ICJ, mwezu huu ilianza kusikiliza faili la kesi ya mauaji ya umati yaliyofanywa na wanajeshi wa Myanmar mwaka 2017 dhidi ya Waislamu Warohingya ambayo iliwasilishwa katika mahakama hiyo na serikali ya Gambia kwa niaba ya nchi 57 za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

3873707

Name:
Email:
* Comment: