IQNA

Msichana kutoka UAE atimiza ndoto yake, ajenga msikiti Uganda

17:33 - February 12, 2020
Habari ID: 3472465
TEHRAN (IQNA) - Msichana kutoka katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ametimiza ndoto yake ya kujenga msikiti katika nchi masikini.

Msichana raia wa UAE mwenye umri wa miaka 15 kwa jina la Rawdha anaugua ugonjwa wa kisukari aina ya 1 na kwa muda mrefu amekuwa na ndoto ya kujenga msikiti katika nchi masikini na msikiti huo upewe jina la marehemu Sheikh Zayed Aal Nahyan, muasisi wa UAE.

Ndoto hiyo ya Rawdha imetimia mapema wiki hii baada  ya Wakfu wa  'Taja Ndoto Yako' , ambao husaidia watu kutimiza ndoto zao, kutangaza kuwa, utatimiza ndoto ya 4,000 kwa kumuwezesha binti huyo kujenga msikiti.  Taasisi hiyo imetangaza kuwa, kwa ushirikiano na Taasisi ya Mohammed bin Rashid Al Maktoum ya Misaada ya Kibinadamu, msikiti unajengwa nchini Uganda kwa niaba ya Rawdha. Kwa mujibu wa ndoto ya Rawdha, msikiti huo utakuwa na uwezo wa kubeba waumini 450 na umepewa jina la Msikiti wa Sheikh Zayed.

Mkurugenzi wa Wakfu wa  'Taja Ndoto Yako', Hani al Zubaidi amesema wana fahari kubwa kuwa, wamesaidia kutumiza ndoto ya 4000 kwa kutoa msaada huo wa kibinadamu.

Baba yake Rawdha ametoa shukrani zake za dhati kwa wakfu huo kwa kumsaidia binti yake kutimiza ndoto yake.

3878286

captcha