IQNA

Jeshi la Yemen latekeleza hujuma ya kihistoria ndani ya Saudi Arabia

12:44 - March 30, 2020
Habari ID: 3472616
TEHRAN (IQNA) - Majeshi ya Yemen yametekeleza oparesheni ya kihistoria na kubwa zaidi ya ulipizaji kisasi ndani ya ardhi ya Saudi Arabia kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora kulenga maeneo muhimu kistratijia katika ufalme huo.

Msemaji wa Jeshi la Yemen Yahya Saree ametoa taarifa na kusema kuwa, kikosi cha makombora na ndege zisizo na rubani cha jeshi kimetekeleza hujuma kubwa zaidi tokea vianzo vita dhidi ya Yemen mwaka 2015. Amesema katika oparesheni hiyo, wamelenga maeneo muhimu ya utawala wa Saudia.

Yahya Saree amesema wameulenga mji mkuu wa Saudia, Riyadh kwa makombora ya Dhul Faqar na ndege isiyo na rubani aina ya Swamad 3. Aidha amesema wamelenga vituo vya kijeshi na kiuchumi katika maeneo ya Jizan, Najran na Asir kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani za Qasef K2.

Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema mashambulizi hayo yametekeleza katika kutekeleza ahadi ya Abdul Malik Badruddin al Houthi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah na ni jibu kwa hujuma za Saudia dhidi ya Yemen.

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia. Zaidi ya watu 16,000 wanaripotiwa kupoteza maisha katika vita vya Saudia dhidi ya Yemen. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel.

3888080

captcha