IQNA

Waislamu Russia watakiwa waswali majumbani Mwezi Mtukufu wa Ramadhani

9:51 - April 09, 2020
Habari ID: 3472647
TEHRAN (IQNA) – Baraza la Maulamaa Russia limetangaza Fatwa mpya inayowataka Waislamu waswali katika majumba yao katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika mwaka huu wa 1441 Hijria Qamaria ili kuzuia kuenea zaidi ugonjwa ambukizi wa COVID-19 au corona.

Kwa mujibu wa taarifa, Baraza la Maulamaa Russia limesema: "Kwa kuzingatia hali ya hivi sasa, ni jambo lisilokubalika kupuuza hatua ambazo serikali ya Russia imechukua kwa ajili ya kuzuia kuenea ugonjwa wa corona." Baraza la Maulamaa Russia limesisitiza kuwa: "Katika misikiti na kumbi za sala  zinazofungamana na baraza hili, hakuna sala ya jamaa itakayosaliwa.

Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Waislamu wa Madhehebu ya Sunni mbali na sala tano pia huswali sala maarufu kama Tarawih kwa jamaa katika misikiti. Baraza la Maulamaa la Russia limesisitiza kuwa sala zote hizo ziswaliwe majumbani na si misikitini katika kipindi chote cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Hadi sasa watu 8,672 wameambukizwa corona nchini Russia huku wengine 63 wakiwa wamefariki dunia.

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema sheria ya kutofanyakazi Russia ili kuzuia kuenea corona imeongezwa hadi Aprili 30.

3890311

captcha