IQNA

Rais wa Ufaransa awahakikishia Waislamu haki zao zitalindwa kipindi cha corona

10:17 - April 09, 2020
Habari ID: 3472648
TEHRAN (IQNA) – Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametoa hakikisho kuwa, Waislamu watakaofariki nchini humo kutokana na ugonjwa wa COVID-19 au corona watazikwa kwa mujibu wa taratibu za Kiislamu.

Mohammad Moussaoui, Rais wa Baraza la Waislamu Ufaransa (CFCM), alimuandikia barua Rais Macron kuhusu matatizo yanayoweza kuibuka kuhusu maziko ya Waislamu. Kufuatia barua hiyo Macron alimpigia simu kujadili wasiwasi walionao Waislamu.

"Rais ametoa hakikisho, pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani Christophe Castaner, kuwa itikadi za kidini zitaheshimiwa wakati wa mazishi ya Waislamu, hata kama itabidi kufanya mipango na maeneo jirani iwapo hakutakuwa na nafasi ya kutosha ya maziko."

Moussaoui amemuuliza Macron kuhusu uvumi kuwa, itakuwa wajibu kuwachoma moto waliofariki, wakiwemo Waislamu, endapo kutakuwa na miili mingi ya kuzikwa.

"Rais amenihakikishia kuwa hilo halitafanyika na kwamba Ufaransa itachukua hatua zote kuheshimu itikadi za kidini kuhusu mazishi," ameongeza Moussaoui. Amesema alisisitiza kuwa, kuchoma maiti ni haramu kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu na Macron akamhakikishia kuwa hilo halitafanyika.

Kati ya watu wote milioni 62 Ufaansa, takribani milioni 5.5 ni Waislamu. Hadi kufikia Aprili 9, watu 112,950 walikuwa wameambukizwa corona nchini Ufaransa na miongoni mwao 10,869 wamepoteza maisha.

3890311

captcha