IQNA

Rais Hassan Rouhani wa Iran

Siku ya Quds Katu Haisahauliki na madhalimu hawataendelea kuikalia kwa mabavu

19:50 - May 20, 2020
Habari ID: 3472785
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kukaribia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kusisitiza kuwa, Quds (Jerusalem) katu haitasahauliwa na haitaendelea kubakia katika uvamizi wa madhalimu.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika kikao na baraza lake la mawaziri na kueleza kuwa, mwaka huu pia katika maadhimisho ya  Siku ya Kimataifa ya Quds wito na sauti ya kudhulumiwa wananchi wa Palestina itawafikia walimwengu kwa njia yoyote ile.

Rais Rouhani amesema kuwa, wananchi wa Iran ya Kiislamu katu hawakubaliani na dhulma na ukandamizaji unaofanywa dhidi ya Wapalestina na hawawezi kulistahamili hilo na bila shaka ushindi wa mwisho utakuwa ni wa wananchi wa Palestina ambao utapatikana kwa kusimama kidete na kwa irada ya chuma ya Wapalestina na hilo litashuhudiwa kwa haraka au kwa kuchelewa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, kila siku Marekani imekuwa ikipanga njama mpya dhidi ya Waislamu na wananchi wa Palestina na kueleza kwamba, ni kwa zaidi ya miaka 70 sasa ambapo wananchi wa Palestina wamekuwa wakimbizi.

Aidha amesema kuwa, kusimama kidete mbele ya mabeberu na madhalimu na wakati huo huo kuwaunga mkono na kuwatetea wanyonge ni katika misingi mikuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Kadhalika Rais wa Iran ameeleza kuwa, madola makubwa ulimwenguni kinara wao akiwa Marekani yamekuwa yakiwaunga mkono na kuwatetea madhalimu, Wazayuni na ubaguzi wa rangi na daima madola hayo yamekuwa yakifanya njama dhidi ya wanyonge na madhulumina, lakini mwisho wa siku haki bila shaka itapata ushindi mbele ya batili.

3900322

captcha