IQNA

Rais Hassan Rouhani

Siku ya Kimataifa ya Quds ni dhihirisho la istiqama na umoja wa Waislamu

12:28 - May 22, 2020
Habari ID: 3472790
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameielezea Siku ya Kimataifa ya Quds inayoadhimishwa hii leo kote duniani kama utamaduni mzuri na nembo ya uvumilivu, umoja na mshikamano wa Waislamu katika kuhami na kutetea thamani za Kiislamu.

Rais Rouhani alisema hayo jana Alkhamisi katika ujumbe wake alioutoa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds na kueleleza bayana kuwa, "licha ya kuwa ni vigumu mwaka huu kufanya marasimu ya kuadhimisha siku hii kutokana na janga la corona, lakini jambo la msingi ambalo linaipa maana halisi kadhia ya Palestina na ukombozi wa Quds Tukufu, sambamba na kutia wahaka kwenye nyoyo za walioghusubu Qibla cha kwanza cha Waislamu, ni uwepo wa kiroho na kuwa na irada thabiti ya kukombolewa Quds, na bila shaka ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu zitakombolewa kwa Rehema ya Allah. Ameongeza kuwa, "bila shaka ushindi mkubwa ni kwa wale wanaopambana na wanaosubiri."

Dakta Rouhani ameashiria kuhusu umuhimu wa umoja na mshikamano wa umma wa Kiislamu na kubainisha kuwa, "naliombea taifa hili kubwa umoja na mshikamano hususan wakati huu ambapo madola ya kiistikbari yameazimia kuwawekea vizingiti vingi wananchi wa Iran, ili kuwakatisha tamaa na kuwafanya washindwe kutekeleza thamani za Kiislamu; kutokana na wimbi la vikwazo, vitisho visivyo vya kiutu na kuanzisha vita vya kiuchumi dhidi ya taifa hili."  Hata hivyo amesisitiza kuwa katu taifa kubwa la Iran haliwezi kupigishwa magoti na Marekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei anatazamiwa leo Ijumaa kutoa hotuba yake kwa njia ya video kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds. Hotuba hiyo itakayoanza saa sita adhuhuri kwa saa za hapa nchini Iran itapeperushwa hewani mubashara na radio na televisheni za ndani na nje ya Iran, na pia katika mitandao ya kijamii.

Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Khomeini (MA) ndiye aliyeipa siku hiyo ya Ijumaa ya mwisho ya mwezi Ramadhani jina la Siku ya Kimataifa ya Quds kwa shabaha ya kuakisi dhulma ya kihistoria inayofanywa na Israel, kwa himaya ya madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, dhidi ya watu wanaoendelea kudhulumiwa na kukandamizwa wa Palestina na ardhi yao takatifu.

Tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, Siku ya Kimataifa ya Quds imekuwa ikiadhimishwa kupitia maandamano na makongamano kote duniani, lakini mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika zaidi kwenye mitandao ya kijamii kutokana na janga la kimataifa la corona.

3900667

captcha