IQNA

Sayyed Hassan Nasrallah

Uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo unaashiria nguvu za muqawama

15:30 - May 27, 2020
Habari ID: 3472806
TEHRAN (IQNA) - Kaitbu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo umetokana na kuimarika nguvu za harakati za mapambano ya Kiislamu au muqawama.

Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameyasema hayo katika mahojiano na Radio Noor siku ya Jumanne kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 20 wa kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon ambalo lilikuwa limekaliwa kwa mabavu na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel. Jeshi hilo la Kizayuni lililazimika kuondoka kwa madhila kusini mwa Lebanon mnamo Mei 25 mwaka 2000.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ilikuwa ni kuhusu sababu ya uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo. Marekani ina idadi kubwa ya majeshi katika eneo la Asia Magharibi na hata inakata kuondoa majeshi yake Iraq pamoja na kuwa Wairaqi wanasisitiza majeshi hayo ajinabu yaondoke. Sababu kuu ya kuwepo majeshi ya Marekani katika eneo ni kuulinda utawala wa Kizayuni wa Israel.

Sayyid Hassan Nasrallah amelitazama suala hili kwa muelekeo mwingine na anaamini kuwa,  kuimarishwa nafasi ya harakati za muqawama katika eneo la Asia Magharibi ni jambo ambalo limepelekea kudhoofika na kuingiwa na kiwewe utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi tegemezi za Kiarabu. Ni kwa sababu hii ndio Marekani inasisitiza kuwepo wanajeshi wake katika eneo ili kulinda usalama wa utawala wa Israel na tawala za Kiarabu ambazo ni vibaraka wake.

Aidha amesema utawala wa Kizayuni wa Israel utasambaratika na kuangamia na kwamba matukio yote yanayoshuhudiwa hivi sasa katika eneo la Asia Magharibi yapo dhidi ya maslahi ya utawala huo pandikizi.

Huku akiutaja utawala wa Israel kama saratani, Sayyid Nasrallah ameonya kuhusu njama za Tel Aviv za kuunda 'taifa la Palestina' nchini Jordan akisisitiza kuwa, mpango huo unakusudia kupora ardhi zote za Wapalestina.

Kadhalika Sayyid Nasrallah sambamba na kuashiria kuhusu mpango wa kibaguzi wa "Muamala wa Karne" amelaani vikali uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa kupora na kuteka ardhi zaidi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Aidha Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameeleza bayana kuwa: Uwepo majeshi ya Marekani katika eneo unaashiria wazi udhaifu wa waitifaki wa Washington na nguvu kubwa ya mrengo wa muqawama.

Itakumbukuwa kuwa, tarehe 25 Mei 2000, utawala wa Kizayuni licha ya kuwa na nguvu za kijeshi, ulisalimu amri mbele ya wanamapambano wa Kiislamu wa Lebanon na ulilazimika kukimbia kwa madhila kusini mwa nchi hiyo. Kila mwaka wananchi wa Lebanon wanaadhimisha siku hiyo ya kukimbia wanajeshi wa mwisho wa Israel kusini mwa nchi yao na siku hiyo wanaiita "Siku ya Muqawama na Ushindi."

3901439

captcha