IQNA

Qalibaf amechaguliwa na wabunge kuwa Spika wa Bunge la Iran

12:12 - May 28, 2020
Habari ID: 3472810
TEHRAN (IQNA) - Mohammad Bagher Qalibaf amechaguliwa kuwa spika mpya wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran. Kikao cha kumchagua spika wa bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu kimefanyika Alhamisi asubuhi.

Qalibaf amechaguliwa na wabunge kuwa  Spika wa Bunge la Iran

Katika kikao hicho, wabunge wa Bunge la 11 mapema leo asubuhi wamefanya kikao cha wazi na kumchagua Mohammad Bagher Qalibaf kuwa spika mpya kwa kura 230 za ndio kati ya kura zote 264.

Sayyid Mostafa Agha Mirsalim na Fereidoun Abbasi ambao walishiriki katika mchuano huo wamepata kura 12 na 17 kwa utaratibu.

Kikao hicho cha bunge la Iran kimewachagua pia Sayyid Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi na Ali Nikzad kuwa Manaibu Spika wa Kwanza na wa Pili wa bunge hilo la 11 la Jamhuri ya Kiislamu.

Uchaguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulifanyika tarehe 21 Februari mwaka huu kwa ajili ya kuchagua wabunge 290 katika majimbo 208 ya uchaguzi kote nchini Iran. Zaidi ya watu milioni 24 na laki tano waliotimiza masharti ya kupiga kura walishiriki kwenye uchaguzi huo.

Kati ya majimbo hayo 208, wabunge wa majimbo 197 walipatikana katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo na uchaguzi wa majimbo 11 tu ndio ulioingia katika duru ya pili ambayo inatarajiwa kufanyika tarehe 11 Septemba mwaka huu.

Qalibaf aliwahi kuwa Meya wa Mji wa Tehran kuanzia mwaka 2005 hadi 2017 na kabla ya hapo alikuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuanzia mwaka 2000 hadi 2005. Kabla ya hapo Qalibaf alihudumu kama kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC). Qalibaf, 58, pia amewahi kugomea kiti cha urais wa Iran mara mbili.

3901642

captcha