IQNA

Rais Rouhani amkosoa Rais Trump wa Marekani kwa kutumia Biblia kuhalalisha jinai na ukatili

21:27 - June 04, 2020
Habari ID: 3472836
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kutumia kitabu cha Biblia kwa ajili ya kuhalalisha jinai na ukatili wa serikali yake na kuwahadaa Wamarekani.

Akizungumza mjini Tehran Alhamisi hii, Rais Rouhani amesema: "Biblia haiamuru kufanya mauaji ya watu wasio na hatia na ni aibu kuona rais anayekandamiza raia wake wa Marekani akishika mkononi kitabu cha Injili." Aidha  amesisitiza kuwa Waislamu wanaiheshimu Injili na Nabii Issa Masiih yaani Yesi-Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran halikadhalika ametangaza mshikamano wake na raia wa Marekani na kusema: "Mienendo ya serikali ya Marekani na ikulu ya rais wa nchi hiyo, White House ambayo ndiyo iliyotoa amri ya kufanyika jinai hizi, inapaswa kulaani."   

Rais Rouhani amesema kuwa Iran inalaani jinai zinazofanywa na serikali ya Marekani na ukandamizaji wake dhidi ya wapinzani wa ubaguzi wa rangi nchini humo.

Amesema maandamano ya sasa ya Wamarekani dhidi ya ubaguzi wa rangi ni kielelezo kwamba, Marekani imo katika kipindi kibaya zaidi cha historia yake na kuongeza kuwa, raia weusi au wenye asili ya Afrika wanasumbuliwa na dhulma kubwa nchini humo.

Ameashiria mauaji yaliyofanywa na polisi wa Marekani dhidi ya raia mwenye asili ya Afrika, George Floyd, na kusema kuwa hii ni kadhia ya kimataifa inayoonesha mshikamano baina ya wanadamu. Amesema tukio hilo linaonesha kwamba, dunia bado ina njia ndefu hadi kufikia kwenye ustaarabu uliosisitizwa na Mitume wa Mwenyezi Mungu.

Siku chache baada ya Rais Trump kuonekana amesimama mbele ya kanisa la St John Episcopal akiwa ameshikilia Bibilia, zaidi ya viongozi 20 wa makanisa kutoka Washington na maeneo yaliyo karibu wamepinga kile alichokifanya.

Kasisi George C Gilbert Senior ambaye ni mmoja wa viongozi hao, aliuambia umati wa watu uliokuwa umekusanyika hapo, kwamba rais alitumia Bibilia "kama chombo cha kuendeleza ajenda yake binafsi".

Itakukumbukwa kuwa nchini Afrika kusini, makaburi walitumia Bibilia kuhalalaisha vitendo vyao vya kuwabagua Waafrika wazalendo kwa misingi ya rangi katika enzi ya utawala wa kibaguzi.

3810208

captcha