IQNA

Spika wa Bunge la Iran atumia aya ya Qur'ani Tukufu kumjibu Trump

13:22 - June 06, 2020
Habari ID: 3472843
TEHRAN (IQNA) - Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ameashiria ujumbe wa Twitter wa Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ametoa pendekezo la kufanyika duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia na Tehran na kusisitiza kuwa, mapambano ya Kiislamu au muqawama ndio njia pekee ya kumshinda adui.

Mohammad Baqer Qalibaf amejibu pendekezo hilo la Trump ambaye Mei 2018 alichukua uamuzi wa upande mmoja wa kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, kwa aya ya 35 ya Suratu Muhammad inayosema:

«فَلَا تَهِنُوا وَتَدْعُوا إِلَى السَّلْمِ وَأَنْتُمُ الْأَعْلَوْنَ وَاللَّهُ مَعَكُمْ وَلَنْ يَتِرَكُمْ أَعْمَالَكُمْ»

"Basi msiregee na kutaka suluhu, maana nyinyi ndio mtakao shinda. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi, wala hatakunyimeni malipo ya vitendo vyenu."

Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Trump mbali na kuishukuru Iran kwa kumuachilia huru Michael White, mfungwa wa Kimarekani aliyekuwa akishikiliwa hapa nchini, amesema, "msisubiri hadi baada ya uchaguzi wa Marekani ili kufikia mapatano makubwa. Nitashinda (uchaguzi). Mtafikia makubaliano bora hivi sasa." 

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif  amemjibu Trump katika ujumbe wa Twitter kwamba: "Ni juu yako wewe (Trump) kuamua ni wakati gani utarekebisha makosa yako ya kujiondoa kwenye mapatano ya JCPOA."

Iran imekuwa ikisisitiza kwamba, Tehran haitafanya mazungumzo yoyote na Marekani hadi pale Washington itakaporejea kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA, iiombe radhi Iran na kuifutia vikwazo vya kidhalimu.

/3903129/

captcha