IQNA

Watu watano wauawa katika hujuma za kigaidi Somalia

18:06 - July 04, 2020
Habari ID: 3472927
TEHRAN (IQNA) – Watu wasiopungua watano wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa kufuatia hujuma za kigaidi nchini Somalia.

Katika hujuma ya kwanza mapema Jumamosi, bomu limelipuka katika kituo cha kukusanya kodi katika eneo la Hamar Jajab mjini  Mogadishu.

Taarifa zinasema hujuma hiyo imetekelezwa na gaidi ambaye aliendesha gari lake lililosheheni bomu kuelekea katika kituo cha polisi cha upekuzi barabrani. Imedokezwa awali gaidi huyo aliwafyatulia risasi polisi ambao nao walijibu kwa kummiminia risasi na hapo gari lake likalipuka. Watu saba wanaripoti kuuawa katika hujuma hiyo akiwamo afisa wa polisi huku gaidi aliyehusika akiangamia papo hapo.

Kwingineko huko Baidoa, mji mkuu wa eneo la kusini magharibi la Bay, bomu la kutegwa ardhini lililipuka karibu na mghawa ulio nje ya mji huo na kupelekea watu watano kupoteza maisha na wengine 10 kujeruhiwa. Hakuna kundi lololte lililotangaza kuhusika na hujuma hizo lakini kundi la kigaidi la Al Shabab, linalofungamana na mtandao wa Al Qaeda hutekeleza mashambulizi kama hayo mara kwa mara nchini Somalia.

Somalia ilitumbukuia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe karibu miaka 30 iliyopita na magaidi wakufurishaji wa Al Shabab walianzisha hujuma dhidi ya nchi hiyo mwaka 2008.

Askari wa Kulinda Amani wa  Umoja wa Afrika Somalia (AMISOM) wapatao 21,000 wamejitahidi kurejesha utulivu katika nchi hiyo lakini hawajafanikia kuliangamiza kundi la kigaidi la Al Shabab ambalo hutekeleza mashambalizi hatari mara kwa mara nchini humo hasa katika mji mkuu Mogadishu.

3471879/

captcha