IQNA

Sheikh Mkuu wa Al Azhar

Kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu ni jinai ya kigaidi

11:35 - September 06, 2020
Habari ID: 3473143
TEHRAN (IQNA) – Sheikh Mkuu wa Al Qur’ani amelaani vikali vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu na kutaja vitendo hivyo vilivyo dhidi ya dini kuwa ni jinai ya kigaidi.

Sheikh Ahmad Tayyib, Sheikh Mkuu wa Al Azhar ameandika katika kurasa zake za mitandao ya kijamii kwamba wale waliothubutu kuteketeza moto nakala ya Qur’ani wafahami kuwa kitendo hicho cha kibaguzi na kilichojaa chuku kinapingwa na tamaduni zote za wanadamu.

Katika taarifa nyingine, Sheikh wa Al Azhar  amesema kumtusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW katu siyo uhuru wa kutoa maoni na akasisitiza kwamba, hatua hiyo ni wito wa kuleta mifarakano.

Sheikh Tayyib amesema: “Mtume wetu ana thamani kuliko roho zetu na kumvunjia heshima mbora huyo wa viumbe huo siyo uhuru wa kutoa maoni, bali ni wito wa wazi wa kuzusha mifarakano, utumiaji mabavu na kuachana na thamani zote za kibinadamu na kistaarabu.”

Sheikh Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar cha nchini Misri amesema kuwa, kuhalalisha kitendo hicho kibaya kwamba, eti ni uhuru wa kutoa maoni ni udriki finyu wa tofauti baina ya haki ya mtu ya kuwa na uhuru, na jinai dhidi ya haki ya mwanadamu kwa jina la kulinda uhuru.

Hivi karibuni, watu wenye chuki dhidi ya Uislamu walichoma moto na kuteketeza nakala ya Qur'ani katika mji wa Malmo nchini Sweden. Walioivunjia heshima Qurani Tukufu nchini Sweden ni wafuasi wa mwanasiasa mwenye misimamo mikali ya kibaguzi wa Denmark, Rasmus Paludan.

Hivi karibuni, watu wenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu walifanya maandamano katika mji mkuu wa Norway, Oslo huku mmoja wao akionekana akichana kurasa za Qurani Tukufu na kuzitemea mate.

Aidha, wafuasi wa mwanasiasa Rasmus Paludan, ambaye anaongoza chama cha chenye misimamo mikali cha mrengo wa kulia ambacho kinapinga Waislamu huko nchini Sweden, walijumuika kinyume cha sheria mjini Malmo na kukivunjia heshima Kitabu Kitukufu cha Waislamu.

Si hayo tu, lakini pia gazeti la maadui wa Uislamu la Charlie Hebdo la nchini Ufaransa, siku ya Jumanne iliyopita lilifanya utovu wa adabu mpya wa kuchora vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW. Vitendo hivyo ambavyo vimefanyika katika fremu ya chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) vinaendelea kulaaniwa kote duniani.

3920438

captcha