IQNA

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Trump! usitie shaka kuhusu kisasi chetu, hilo ni jambo lisilo na shaka na ni ukweli mtupu

17:36 - September 19, 2020
Habari ID: 3473185
TEHRAN (IQNA) - Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema hakuna chembe ya shaka kwamba Iran italipiza kisasi cha kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC.

Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo mapema leo Jumamosi na kubainisha kuwa, Jeshi la IRGC litachukua hatua kali ya kulipiza kisasi cha mauaji hayo ya kigaidi. Amemhutubu Rais Donald Trump wa Marekani kwa kumuambia: Trump! usitie shaka kuhusu kisasi chetu, hilo ni jambo lisilo na shaka na ni ukweli mtupu."

Hata hivyo Meja Jenerali Hossein Salami amesisitiza kuwa, kisasi cha taifa hili kwa mauaji ya Soleimani kitawalenga tu waliohusika kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Amehoji: "Unadhani tutaua balozi mwanamke mkabala wa damu ya ndugu yetu aliyeuawa shahidi? Sisi ni watu wenye heshima, na kisasi chetu pia ni cha kiuadilifu, ndiposa hatukuwalenga wanajeshi wenu Ainul Assad."

Januari 3 mwaka huu, jeshi la kigaidi la Marekani kwa amri ya rais wa nchi hiyo Donald Trump lilimuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani karibu wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Iraq, na siku tano baadaye, vikosi vya Iran vilivurumisha makombora ya belestiki na kupiga kambi ya kijeshi ya Marekani ya Ainul Assad nchini Iraq. Washington inadai kuwa, Iran inapanga kumuua Lana Marks, Balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini eti kama kisasi cha mauaji ya Soleimani, tuhuma ambazo zimekanushwa vikali si tu na Iran, bali hata na Afrika Kusini.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, hii leo Marekani imepoteza dira na hisa kubwa ya ushawishi wake duniani, kwa kuwa kuna nguvu mpya zinazochipukia duniani, kama vile 'Uislamu kama nguvu ya ustaarabu' ambao umevunja ubeberu wa Marekani.

Jenerali Salami ameongeza kuwa, Marekani imetengwa kisiasa hii leo na mfano hai ni nanma ilivyopigwa mweleka katika azma yake ya kutaka kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran. Ameeleza bayana kuwa, "Rais Donald Trump alishindwa kuwashawishi hata waitifaki wa kawaida wa Marekani, ghairi ya Jamhuri ya Dominican. Kilichobaki kwa Marekani hivi sasa ni moshi, moto, na kuvunja hadhi ya mwanadamu katika mitaa, na kufeli kwa mfumo, na Marekani hiyo hiyo inatishia Iran."

3923797

captcha