IQNA

Kiongozi wa Hizbullah aonya kuhusu njama ya Marekani kuhuisha tena kundi la kigaidi la ISIS

11:14 - September 30, 2020
Habari ID: 3473216
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema magaidi wa Marekani walilenga kuhusisha kundi la kigaidi la ISIS walipowaua shahidi Luteni Jenerali Haj Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Kamanda wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq (Hashd al Shaabi).

Sayyid Hassan Nasrallah, Kiongozi wa Hizbullah ameyasema hayo katika hotuba kwa njia ya televisheni Jumanne usiku na kuongeza kuwa, baada ya oparesheni ya kigaidi ya Marekani iliyopelekea kuuawa shahidi Haj Soleimani na Al Muhandis, kundi la kigaidi la ISIS au Daesh lilianza kuhuishwa. Ameongeza kuwa, lengo la Marekani katika kuhuisha ISIS  ni kujaribu kutetea kuendelea kuwepo wanajeshi wake katika eneo.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameashiria pia uingiliaji wa Ufaransa katika mambo ya ndani ya Lebanon na kusema: "Kile ambacho Ufaransa inataka Lebanon ni kuondolewa madarakani wawakilishi wa waliowengi na kuchukua hatamu wawakilishi wa waliowachache."

Sayyid Hassan Nasrallah hali kadhalika ameashiria hatua ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema, wananchi hawako pamoja na serikali zao katika kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.

Katibu Mkuu wa Hizbullah aidha amelitaka taifa la Sudan liangazie historia yake ya mapambano na hivyo lisiruhusu kurejea tena chini ya satwa ya mabeberu kwa visingizo kama vile ugaidi na masuala ya kiuchumi.

Nasrallah pia amezishukuru serikali za Tunisia na Algeria kwa msimamo wao wa kupinga uanzishwaji uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel. Ameongeza kuwa wale walioanzisha uhusiano na utawala huo hivi karibuni watafahamu kosa kubwa walilofanya.

3472680

captcha