IQNA

Walowezi wa Kizayuni wauhujumu Msikiti wa Al Aqsa

19:57 - October 16, 2020
Habari ID: 3473265
TEHRAN (IQNA) – Makumi ya walowezi wa Kizayuni siku ya Alhamisi waliuhujumu uwanja wa Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) wakiwa wanalindwa na askari wa utawala haramu wa Israel ambapo wametekeleza ibada za Kiyahudi katika eneo hilo takatifu la Waislamu.

Idara ya Wakfu wa Kiislamu mjini Quds imesema walowezi hao wachochezi wa Kizayuni wamezunguka kiholela katika eneo la kaskazini katika msikiti huo huku wakilindwa na askari wa Israel.

Mara kwa mara walowezi wa Kizayuni huuvamia Msikiti wa al-Aqsa  wakisaidiwa na askari wa jeshi la utawala haramu wa Israel na kuuvunjia heshima msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za kukabiliana na vitendo hivyo.

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya njama za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.

Msikiti wa al-Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu umekuwa ukiandamwa na njama mtawalia za utawala vamizi wa Israel, hatua ambazo zinakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.

3472843

captcha