IQNA

Dunia yaendelea kumlaani Rais wa Ufaransa kutokana na chuki zake dhidi ya Uislamu

11:18 - October 26, 2020
Habari ID: 3473297
TEHRAN (IQNA) -Malalamiko na ukosoaji dhidi ya matamshi yaliyotolewa na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akitetea vitendo vya kutusiwa na kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW nchini humo unaendelea kupamba moto huku nchi mbalimbali za Kiislamu zikitoa wito wa kuiadhibu Paris kwa kususia bidhaa za Ufaransa.

Katika uwanja huo Rais Emmanuel Macron alijitokeza tena jana bila ya soni na kutetea tena matusi na kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu kwa kuandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba, Paris haitalegeza kamba wala kurudi nyuma. 

Rais wa Ufaransa amedai kuwa, hakubali matamshi yanayochochea chuki na kwamba anatetea mijadala ya kimantiki.

Ususiwaji bidhaa za Ufaransa

Wakati huo huo Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ufaransa imetoa taarifa ikizitaka nchi za Waislamu kusitisha wito wa kususiwa bidhaa za nchi hiyo baada ya Rais Macron kutetea matusi na vitendo vya kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad (saw) katika jarida la Charlie Hebdo la nchi hiyo. 

Kwa sasa trend inayotamba katika mitandao ya kijamii kwenye nchi za Kiislamu ni ile ya "#Susia Bidhaa za Ufaransa" kama jibu la awali dhidi ya matamshi ya rais wa nchi hiyo ya kutetea matusi na kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW.

Imran Khan atoa kauli 

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan ametaka mkuu wa mtandao wa kijamii wa Facebook Mark Zuckerberg apige marufuku uchapishaji wa maudhui zote ambazo zinaeneza chuki dhidi ya Uislamu.

Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter, Imran Khan amesema: "Kwa kuzingatia matusi dhidi ya Waislamu katika mitandao ya kijamii, nakuomba upige marufuku maudhui zenye chuki dhidi ya Uislamu katika Facebook kama ambavyo umepiga marufuku maudhui za wanaokana kuwepo Holocaust (mauaji ya Mayahudi huko Ujerumani).

Waziri Mkuu wa Pakistan amesema sasa kuna vitendo vingi vya chuki dhidi ya Waislamu duniani. Ameashiria uchapishwaji wa vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na ubaguzi mkubwa dhidi ya Waislamu nchini India.

Imran Khan amebainisha masikitiko yake kuwa hivi sasa nchini Ufaransa Uislamu unanasibishwa na ugaidi na kuongeza kuwa hatua hiyo itaibua mgawanyiko katika jamii na kupelekea Waislamu watengwe zaidi nchini humo. Waziri Mkuu wa Pakistan pia amemkosoa vikali Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa kutoa matamshi yenye chuki dhidi ya Waislamu.

Amesema, "sifa kuu za kiongozi ni kuwaunganisha wanaadamu kama alivyofanya Mandela. Huu ni wakati ambao Rais Macron angepaswa kuutumia kutuliza mambo na kuwanyima fursa wenye misimamo mikali."

Imran Khan amesikitika kuwa Macron ameamua kuendelea kuhimiza chuki dhidi ya Uislamu kwa kuushambulia Uislamu badala ya kukabiliana na magaidi wawe ni Waislamu, wazungu wenye itikadi kuwa wao ni bora au Wanazi.

Imran Khan ameongeza kuwa: Macron amehujumu Uislamu baada ya kuhamasisha vibonzo vinavyomtusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.

Rais Erdogan asema Macron apimwe akili

Kwa upande wake Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa Rais wa Ufaransa, Emanue Macron, anahitaji kupimwa uwezo wake wa kiakili baada ya matamshi ya kibaguzi aliyotoa karibuni kuhusu dini ya Uislamu.

Recep Tayyip Erdoğan amehoji: "Ni kitu gani tunaweza kusema kuhusiana na rais wa nchi asiyejua maana ya uhuru wa itikadi na anaamiliana na mamilioni ya wafuasi wa dini tofauti (Uislamu) nchini kwake kwa njia kama hii?"

Rais wa Uturuki amesema: "Hivi kweli Rais Macron wa Ufaransa ana tatizo gani na Uislamu na Waislamu? Anahitaji kupewa matibabu ya matatizo ya akili". 

Muhammad Ali al Houthi amelaani vikali kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW nchini Ufaransa na amezitaka nchi za Kiislamu kuitisha kikao rasmi cha kulaani uhalifu huo.

Mashirika na maduka makubwa katika baadhi ya nchi za Kiislamu kama Kuwait na Qatar tayari yameanza kutekeleza wito wa kususiwa bidhaa za Ufaransa kama hatua ya mwanzo na kuitia adabu Paris baada ya rais wa nchi hiyo kutetea uovu wa kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad- Rehema na Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake na Kizazi Chake Kitoharifu- SAW.

3931251

captcha