IQNA

Miinuko ya Golan hatimaye itarejeshewa Syria

22:29 - November 21, 2020
Habari ID: 3473381
TEHRAN (IQNA) – Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Ayman Sousan amemlaani vikali Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo kwa kutembelea Miinuko ya Golan ya Syria ambayo inakaliwa kwa mabavu na Israel na kusema ardhi hiyo hatimaye itarejea Syria.

Akizungumza na Televisheni ya Al Manar, Sousan amesema hatua ya Pompeo kutembelea eneo linalokaliwa kwa mabavu ni sawa na kukaidi sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Amesisitiza kuwa Miinuko ya Golan ni milki ya Syria na jamii ya kimataifa inapinga hatua ya Marekani ya kutambua kuwa eti utawala bandia wa Israel nidio mmiliki wa miinuko hiyo.

Siku ya Jumatano Pompeo alifika Tel Aviv na kisha akaelekea katika miinuko ya Golan. Syria imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kulaani safari hiyo.

Mapema mwezi huu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha kwa wingi wa kura uamuzi wa kuutaka tena utawala haramu wa Israel uondoke katika Miinuko ya Golan ya Syria unayoikalia kwa mabavu. Nchi 142 zimeupigia kura ya ndio uamuzi huo, 19 zikijizuia kupiga kura na kuonekana kura mbili tu za kupinga uamuzi huo ambazo ni za Marekani na utawala hramu wa Israel wenyewe. Nchi wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa uamuzi wao huo kwa mara nyingine tena zimesisitiza kutokuwa halali kukaliwa kwa mabavu na Israel miinuko ya Golan ya Syria.

3473179

Kishikizo: syria golan
captcha