Taarifa za siri zimebaini kuwa baadhi ya wanajeshi wa Australia waliwaua raia wakiwemo watoto ambao hawakuwa na silaha nchini Afghanistan.
Baada ya kufichuliwa kasfha hiyo, wanajeshi tisa wamejiua hivi karibuni na miongoni mwa waliojiua ni mwanamke mmoja na wanaume nane.
Gazeti la The Advertiser limesema walijiua baada ya klipu ya kushtua ya video kuonyesha mwanajeshi wa Australia akimuua raia wa Afghanistan.
Akiwasilisha muhtasari wa ripoti ya uchunguzi wa miaka minne mbele ya waandishi wa habari mjini Canberra hivi karibuni, Mkuu wa Jeshi la Australia Angus Campbell alisema kikosi maalum cha jeshi la Australia kilihusika na mauaji hayo dhidi ya wafungwa, wakulima na raia wa kawaida.
Jenerali Campbell alisema kuna rikodi za kutia aibu kama vile mwanajeshi kumuuwa mfungwa ili tu kupata ladha ya kumuuwa mtu wa kwanza, tendo ambalo kijeshi huitwa "kumwaga damu", na kisha baada ya mauaji kama hayo, wanajeshi walikuwa wakipandikiza silaha na redio ili kutunga madai ya uongo kwamba wahanga wao walikuwa maadui waliouawa kwenye mapambano.
Wanajeshi hao wa Australia walikuwa waliwa nchini Afghanistan chini ya kikosi cha kimatiafa cha ISAF ambacho kinasimamiwa na muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi NATO chini ya uongozi wa Marekani.
Hayo yanajiri wakati ambao Majaji waandamizi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wameamuru uchunguzi uanze kuhusu jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu ambazo zinaripotiwa kufanywa na askari wa Marekani nchini Afghanistan. Afghanistan ilivamiwa
na Marekani pamoja na waitifaki wake mwaka 2001 kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi lakini si tu kuwa ugaidi haujapungua bali hata umeongezeka huku nchi hiyo ikishuhudia mashambulia ya magaidi karibu kila siku.