IQNA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Dalili zinaonyesha Israel imehusika katika mauaji ya mwanasayansi wa Iran

6:12 - November 28, 2020
Habari ID: 3473401
TEHRAN (IQNA) - Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amelaani vikali hujuma hiyo ya kigaidi na kuongeza kuwa, kuna dalili nzito zinazoonyesha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ulihusika katika mauaji ya Mohsen Fakhrizadeh ambaye alikuwa Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu katika Wizara ya Ulinzi ya Iran.

Jana Ijumaa alasiri, Fakhrizadeh aliuawa shahidi baada ya gari lililokuwa limembeba kushambuliwa katika mji wa Absard katika eneo la Damavand mkoani Tehran.

Kwa mujibu wa taarifa, awali gari lililokuwa limesheheni bomu lilirupika na kisha ufyatulianaji risasi ukafuata baina ya walinzi wa shahidi wa Fakhrizadeh na magaidi.

Idara ya Habari katika Wizara ya Ulinzi ya Iran imesema Shahidi Fakhrizadeh, ambaye pia alikuwa profesa wa  fizikia katika Chuo Kikuu cha Imam Hussein mjini Tehran, alijeruhiwa vibaya wakati wa mapigano baina walinzi wake na magaidi na kisha akakimbizwa hospitali na kufariki kufuatia majeruhi yake. Shirika la Habari la Faris limesema watu watatu hadi wanne waliuawa katika mapigano hayo na wote walikuwa ni magaidi.

Katika ujumbe kupitia Twitter, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ameandika: “Magaidi wamemuua mwanasayansi maarufu wa Iran leo. Kuna dalili nzito zinazoonyesha Israel imehusika na ni ishara ya wanavyotapatapa wapenda vita.”

Zarif ametoa wito kwa jamii ya kimataifa, hasa Umoja wa Ulaya kusitisha udumakuwili wenye kuaibisha na kulaani kitendo hiki cha kigaidi.

Naye mwenyekiti wa Kamandi Kuu ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri amesema hujuma hiyo ya kinyama imetekelezwa na magaidi wanaofungamana na uistikbari wa kimataifa na utawala wa kishetani wa Kizayuni. Amesema ingawa mauaji hayo ni pigo kwa viwanda vya ulinzi vya Iran lakini maadui wafahamu kuwa, njia iliyofunguliwa ma wasomi kama Shahidi Fakhirzadeh haiwezi kufika ukingoni.”

Baqeri aidha amesema ulipizaji kisasi mkali unawasubiri waliotekeleza ugaidi huo kwani watafuatiliwa na kufikishwa kizimbani.

3473239

captcha