IQNA

Ujumbe wa mtawala wa Bahrain watembelea msikiti wa Al Aqsa kwa siri

20:54 - November 30, 2020
Habari ID: 3473409
TEHRAN (IQNA)- Mjumbe wa Mfalme wa Bahrain na wenzake aliofuatana nao wameingia msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem), unaokaliwa kwa mabavu na Israel, kwa kujificha wakihofu wasije wakatambuliwa na Wapalestina.

Khalid Aal Khalifa, mwakilishi wa mfalme wa Bahrain amesema katika mahojiano na redio ya jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwamba Ijumaa usiku, akiwa amefuatana na watu wengine kadhaa waliingia ndani ya msikiti wa Al Aqsa kwa kutumia utambulisho bandia na kwamba hawakuthubutu kutangaza utambulisho wao halisi kwa kuwahofu Wapalestina.

Mwakilishi huyo wa mfalme wa Bahrain amekiri kuwa endapo wangejitambulisha wao ni nani Wapalestina waliokuwa wakisali msikitini humo wasingewaruhusu waingie na wangewafukuza.

Kabla ya hapo, ujumbe wa Imarati ulitimuliwa na kutolewa nje ya msikiti wa Al Aqsa na Wapalestina walipotambuliwa baada ya kuingia msikitini humo.

Katika hatua inayopingana kikamilifu na malengo matukufu ya watu wa Wapalestina ya ukombozi wa nchi yao, tarehe 25 Septemba, mawaziri wa mambo ya nje wa Imarati na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mjini Washington na kuhudhuriwa na rais wa Marekani Donald Trump na Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel.

Uamuzi wa nchi hizo mbili ndogo za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi wa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala unaoikalia Quds tukufu kwa mabavu umewaghadhibisha Wapalestina pamoja na wananchi wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu,wakiutaja kuwa ni uhaini na usaliti kwa malengo ya haki ya Palestina pamoja na matukufu ya Kiislamu ya mji Quds, hususan msikiti wa Al Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu kilichopo katika mji huo mtakatifu.

3938238

captcha