IQNA

Umoja wa Mataifa walaani hujuma za kigaidi Baghdad

20:04 - January 22, 2021
Habari ID: 3473582
TEHRAN (IQNA) – Umoja wa Mataifa umelaani hujuma za kigaidi mjini Baghadad ambazo zimepelekea makumi ya watu kuuawa na kujeruhiwa.

Kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) limetangza kuwa ndilo lililohusika na jinai hiyo iliyofanywa kwenye kitovu cha mji mkuu huo wa Iraq.

Bi. Jeanine Hennis-Plasschaert mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq ametoa taarifa na  kulaani vikali hujuma hiyo.

Nayo Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imelaani mashambulio ya kigaidi yaliyotokea jana katika mji mkuu wa Iraq Baghdad na kusisitiza ulazima wa kuweko umoja na mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya kupambana na ugaidi.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imeeleza kuwa, mashambulio haya ya kijinai kwa mara nyingine tena yameweka wazi ukweli huu kwamba, juhudi za kupambana na ugaidi haziwezi kuzaa matunda madhali ugaidi huo haujaangamizwa kikamilifu na hakujawa na umoja na mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya vita hivyo.

Kadhaika taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imebainisha kuwa, ugaidi ungali tishio kwa usalama na uthabiti wa kieneo na ulimwengu kwa ujumla.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa, magaidi wa Daesh (ISIS) wasubiri majibu makali kutoka kwa wananchi na vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo na kusisitiza kwamba serikali yake itahakikisha mashambulizi mengine ya kigaidi hayatokei nchini humo.

Vyombo vya habari vimemnukuu Mustafa al Kadhimi, Waziri Mkuu na Amirijeshi Mkuu wa Majeshi ya Iraq akisema hayo leo Ijumaa katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama wa Taifa la nchi hiyio na kuongeza kuwa, magaidi wametumia upenyo mdogo tu kufanya mashambulizi ya mabomu mjini Baghdad hivyo inabidi vipenyo kama hivyo viondolewe haraka.

Waziri Mkuu wa Iraq vile vile ametaka kutolewe mafunzo bora na kuongezwe uwezo na uimara wa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo akisisitiza kuwa, sasa hivi mji wa Baghdad unafanyia kazi mkakati mkubwa wa kiusalama na wenye taathira katika kukabiliana na changamoto zijazo za kiusalama na kwamba mkakati na stratijia hiyo inasimamiwe moja kwa moja na yeye mwenyewe Waziri Mkuu wa Iraq.

Shambulio hilo la kigaidi limeonyesha kuwa, masalia ya kundi la Daesh yangali ni tishio kubwa la kiusalama kwa Iraq; na kwa kuzingatia aina ya shambulio lenyewe, upo uwezekano wa jinai kama hiyo kurudiwa tena.

Ijapokuwa kuna maombwe mengi ya kiusalama ndani ya Iraq, lakini kushughulishwa na masuala ya uchaguzi kumetoa mwanya kwa mabaki ya kundi la kitakfiri la Daesh (ISIS) kufanya shambulio kubwa la kigaidi kwenye kitovu cha mji mkuu Baghdad. Kuhusiana na nukta hiyo, Naibu wa kwanza wa Spika wa Bunge la Iraq amesema, shambulio hilo limetokana na uzembe na udhaifu wa ufanyaji kazi katika vyombo vya usalama na katika uchukuaji hatua vyombo hivyo za kuzuia hujuma.

3949162/

Kishikizo: baghdad ugaidi isis
captcha