IQNA

Mpango wa kuwawezesha Wanigeria kuweka akiba kugharamia Hija

10:14 - February 23, 2021
Habari ID: 3473677
TEHRAN (IQNA) – Benki moja ya Kiislamu nchini Nigeria imezindua mpango wa kuwahimiza Waislamu kuweka akiba ya fedha za kutumika kwa ajili ya kutekeleza Ibada ya Hija ambayo ni katika nguzo za Uislamu.

Mpango huo umezinduliwa kwa pamoja na Benki ya Jaiz na Tume ya Kitaifa ya Hija Nigeria kwa ushirikiano na Bodi ya Mahujaji kwa lengo la kuwawezesha Waislamu kuweka akiba kwa ajili ya safari ya ibada ya Hija.

Mkurugenzi wa Benki ya Jaiz, Hassan Usman amesema Mpango wa Kitaifa wa Akiba ya Hija ni hatua muhimu ambayo itawasaidia Waislamu kutekeleza nguzo hiyo muhimu ya kidini.

Naye mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Hija Zikrullah Kunle Hassan amezishukuru serikali za majimbo yaliyokubali kuzindua mpango huo.  Amesema lengo lao ni kuwasaidia wasiojiweza kuchanga pesa kwa ajili ya safari ya Hija na pia kupata faida kutokana na akiba yao.

Mpango huo tayari umezinduliwa katika majimbo ya Ebonyi, Taraba na Adamawa.

Mwaka 2019, Wanigeria 95,000 walipata fursa ya kutekeleza ibada ya Hija na hivyo kuianya kuwa nchi ya Afrika yenye idadi kubwa zaidi ya mahujaji.

/3955612

Kishikizo: nigeria hija waislamu
captcha