IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Iran yalenga kustawisha umoja wa Kiislamu

15:23 - March 02, 2021
Habari ID: 3473694
TEHRAN (IQNA) – Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran yanalenga, kati ya mambo mengine, kustawisha umoja na mshikamano wa Kiislamu duniani kote.

Akizungumza katika kikao na waandishi habari mjini Tehran mnamo Machi Mosi kuhusu Mashindano ya 37 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran, Mkuu wa Shirika la Wakfu la Iran Hujjatul Islam Sayyed Mehdi Khamoushi amesema kukurubisha nyoyo za Waislamu kutoka mataifa mbali mbali ni moja ya malengo ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ambayo huandaliwa na Iran kila mwaka.

Amesema lengo jingine la mashindano hayo ni kuinua hadhi ya Qur'ani Tukufu kama kitabu cha maisha na ustawi wa Ummah wa Kislamu duniani. Halikadhalika amesema mashindano hayo ya Qur'ani yanakusudia kuinia hadhii ya wasomaji Qur'ani duniani.

Hujjatul Islam Khamoushi aidha amesema mwaka huu mwashindano hayo yanafanyika kwa njia ya intaneti kutokana na maambukizi ya corona. Amesema nchi nyingi za Kiislamu zimefuta kabisa mashindano yao ya kila mwaka ya Qur'ani kutokana na corona lakini amesema Iran imeamua kuandaa mashindano hayo ya Qur'ani kwa njia ya intaneti.

Fainali za Mashindano ya 37 ya Kimataifa ya Qur'ani zitafanyika Machi 6-11 kwa njia ya intaneti na kurushwa hewani mubashara kupitia Televisheni ya Qur'ani ya IRIB, Radio ya Qur'ani ya IRIB na majukwaa mengine ya mtandaaoni.

Kauli mbiu ya mashindano ya mwaka huu ni 'Kitabu Kimoja, Ummah Mmoja".

Semi fainali ya mashindano hayo imefanyika mapema mwezi huu kwa njia ya intaneti ambapo kulikuwa na washiriki 120 kutoka nchi 70. Duru za awali za mchujo katika mashindano hayo zilikuwa na washiriki 600 kutoka nchi 70 na zilifanyika pia kwa njia ya intaneti kutokana na janga la corona. Washiriki 57 kutoka nchi 26 watashindano katika fainali za mashindano yam waka huu.

Shirika la Wakfu la Iran huandaa mashindano hayo ya kimataifa ya Qur'ani kila mwaka.

Kutokana na janga la COVID-19 mashindano hayo hayakufanyika mwaka 2020 na yalifanyika mara ya mwisho Aprili 2019 mjini Tehran ambapo washiriki kutoka nchi zaidi ya 80 walishiriki.

3956893

captcha