IQNA

Jinai za kivita za Israel dhidi ya Wapalestina zachunguzwa na ICC

12:25 - March 04, 2021
Habari ID: 3473702
TEHRAN (IQNA)- Mwendesha Mashtaka wa Makakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) amesema kuwa mahakama hiyo imeanza uchunguzi kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.

Mkuu wa Mashtaka wa Mahakama ya ICC, Fatou Bensouda, amesema kwamba uchunguzi kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina utakuwa huru na usiopendelea upande wowote.

Mwezi uliopita wa Februari Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitangaza kuwa inao ustahiki wa kushughulikia jinai za kivita za Israel huko Palestina. 

Hatua hiyo ya mahakama ya ICC imewafurahisha sana Wapalestina na kuukasirisha utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imekaribisha uamuzi huo wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na kutangaza kuwa, uamuzi wa ICC wa kuchunguza jinai zilizofanyika katika ardhi za Palestina katika mipaka ya mwaka 1967 ni tukio la kihistoria katika harakati za kuuwajibisha na kuuadhibu utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Marekani tayari imepinga hatua ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya kuanza uchunguzi kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na Israel huko Palestina. 

Siku kadhaa zilizopita, tovuti ya Axius iliwanukuu maafisa wa Kizayuni na kuripoti kuwa, katika mazungumzo ya kwanza ya simu ambayo Benjamin Netanyahu alifanya na Rais Joe Biden wa Marekani, waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni aliitaka Washington iendeleze vikwazo vilivyowekwa na rais aliyetangulia wa nchi hiyo Donald Trump dhidi ya mahakama ya ICC.

Gazeti la Haaretz liliwahi kutoa orodha ya watu ambao kuna uwezekano wa kushtakiwa katika faili la uchunguzi wa jinai za kivita zilizofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ufukwe wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, ambapo katika orodha hiyo yanaonekana pia majina ya viongozi wqa ngaziz a juu wa Israel kama Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, Waziri wa Ulinzi Benny Gantz, mkuu wa zamani wa majeshi ya Israel Moshe Ya'alon, waziri wa zamani wa uchumi Naftali Bennett na Avigdor Lieberman aliyewahi kuwa waziri wa ulinzi wa Israel   

3957502

captcha