IQNA

Papa Francis asikiliza qiraa ya Qur'ani eneo alikozaliwa Nabii Ibrahim nchini Iraq

20:00 - March 07, 2021
Habari ID: 3473714
TEHRAN (IQNA) – Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Jumamosi alisikiliza qiraa ya Qur'ani katika mji wa kale mji wa Ur Kaśdim kaskazini mwa Iraq, eneo ambalo inaaminika alizaliwa Nabii Ibrahim (Abraham) –Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake.

Papa Francis aliyewasili Iraq Ijumaa alihutubia jamii mbali mbali za kidini katika mji wa Ur Kasdim alikozaliwa Nabii Ibrahim, Nabii ambaye Waislamu , Wakristo na Mayahudi, wote kwa pamoja wanamuamini. Akiwa hapo Papa Francis alisikiliza aya za Qur'ani Tukufu zikisomwa.

Wakati huo huo, Papa Francis amesema udugu una nguvu zaidi kuliko mauaji na suluhu ina nguvu zaidi kuliko vita. Ameyasema hayo leo mjini Mosul wakati akiendelea na ziara yake ya siku nne nchini Iraq.

Katika safari yake hiyo huko Mosul, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki ametembelea kanisa la Hushul-Bai'a na katika hotuba yaliyotoa, alizungumzia athari za vita katika mji huo ulioko kaskazini mwa Iraq na kubainisha kuwa, ni jambo la kusikitisha kuona ardhi za staarabu zimekumbwa na hujuma kubwa za kigaidi.

Papa Francis amesema, kupungua idadi ya Wakristo wa Mosul na Mashariki ya Kati kuna madhara makubwa kwa muundo wa kijamii na akazitolea mwito familia za Kikristo kurejea mjini humo na kuanzisha tena shughuli zao za maisha.

Papa Francis amesisitiza pia kuwaombea dua waathirika na kufanya maombi ili kuweza kuishi kwa amani na urafiki.

Baada ya kutembelea mjini Mosul, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani alielekea mji wa Qaraqosh mkoani Nainavah, eneo lenye idadi kubwa zaidi ya Wakristo nchini Iraq ambako alipata mapokezi makubwa ya watu wa mji huo.

Papa Francis alitazamiwa pia kufika kwenye kanisa la T'ahiratul-Kubra mjini Qaraqosh, ambalo ni moja ya makanisa makubwa zaidi nchini Iraq na kuongoza misa maalumu.

Katika safari yake nchini Iraq, Kiongozi wa Kanisa Katoliki amekutana pia na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Juu wa Kidini (Marjaa Taqlid) nchini humo Ayatullah Ali Sistani.

/3474176

captcha