IQNA

Waislamu Ufaransa walalamikia marufuku ya nyama ‘Halal’

12:55 - March 20, 2021
Habari ID: 3473749
TEHRAN (IQNA) – Waislamu nchini Ufaransa wamelalamikia hatua ya wakuu wan chi hiyo kupiga marufuku uchinjaji wa kuku kwa misingi ya Kiislamu huku mwezi Mtukufu wa Ramadhani ukikaribia.

Mkurugenzi wa Msikiti wa Paris Chems-eddine Hafez, mkurugenzi wa Msikiti wa Lyon Kamel Kapatano na mkurugenzi wa Msikiti wa Evry wametoa taarifa ya pamoja na kusema amri ya Wizara na Kilimo na Chakula Ufaransa ya kupiga marufuku uchinjaji wa kuku kwa misingi ya Uislamu ni jambo ambalo linatoa ishara hasi kwa Waislamu nchini humo  katika kipindi hiki cha kukaribia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Wamesema wamelalamikia uamuzi huo wa mwezi Novemba mwaka jana lakini bado hawajapokea jibu lolote.

Ufaransa imeungana na baadhi ya nchi za Ulaya kama vile Ubelgiki kupiga marufuku uchinjaji wa nyama kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu. Aidha katika kitendo kinachoashiria chuki ya wazi dhidi ya Waislamu supamaket moja ya Paris imelazimiwa na wakuu wa mji huo kuuza nyama ya nguruwe na pombe, bidhaa  ambazo ni haramu kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu. Supamaket hiyo inyojulikana kama 'Good Price' iliyo katika mtaa wa Colombes mjini Paris ilifahamishwa kuwa leseni yake itabatilishwa iwapo haitatii amri ya kuuza pombe na nyama na nguruwe.

Hayo yanajiri baada ya  Bunge la Ufaransa kuidhinisha sheria iliyo dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, ambayo imepewa jina la “Sheria ya Kuimarisha Thamani za Kijamhuri” inalenga kukabiliana na mambo kadhaa yanayowahusu Waislamu kama vile mafunzo ya kidini, mitandao na kuoa wake wengi.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amependekeza sheria hiyo kwa ajili ya kukabiliana na kile alichokitaja ni 'Uislamu wa wanaotaka kujitenga.'

Msimamo huo wa Rais Macron umetajwa kuwa moja ya sababu ambazo zinachochea chuki dhidi ya Uislamu Ufaransa.

3960723

captcha