IQNA

Saudia yasema sharti la Umrah ni chanjo ya COVID-19

22:32 - April 06, 2021
Habari ID: 3473788
TEHRAN (IQNA)- Ufalme wa Saudi Arabia umesema Waislamu wanaokusudia kutekeleza ibada ya Umrah katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ni sharti kwanza wapate chanjo ya COVID-19 au corona.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Hija ya Saudia imesema kuwa, watu waliopata dozi mbili za chanjo ya corona au wale waliopitisha siku 14 tangu baada ya kupewa dozi ya kwanza au walioumwa na kupona corona, ndio watakaoruhusiwa kutekeleza ibada ya umra katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, ruhusa ya kufanya ibada ya Umrah, kutekeleza Swala katika Masjidul Haram huko Makka na kuzuru Msikiti wa Mtume mjini Madina itaanza kutolewa mwanzoni mwa mwezi wa Ramadhani. 

Oktoba mwaka jana Saudi Arabia ilifungua tena milango ya Msikiti mtakatifu wa Makka kwa ajili ya Swala baada ya kufungwa kwa kipindi cha miezi 7 kutokana na hofu ya maambukizi ya corona. 
Mwaka jana pia Saudia Arabia ilizuia ibada ya Hija kwa wahujaji wote kutoka nje ya nchi hiyo na kuruhusu watu elfu 10 tu wa ndani kutekeleza ibada hiyo muhimu ya Kiislamu. 

Maelfu ya Wasaudia wamepoteza maisha hadi sasa kutokana na ugonjwa wa Covid-19.  

Tayari wakuu wa Saudia wameshatangaza kuwa sharti la kutekeleza ibada ya Hija litakuwa ni kupata chanjo ya COVID-19.

3474378

Kishikizo: umrah saudia covid 19
captcha