IQNA

Wapalestina takribani laki moja katika Sala ya Idul Fitr Msikiti wa Al Aqsa

20:21 - May 13, 2021
Habari ID: 3473906
TEHRAN (IQNA)-Wapalestina karibu laki moja wameshiriki katika Sala ya Idul Fitr leo Alkhamisi asubuhi katika Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu katika mji wa Quds (Jerusalem) licha ya sheria kali zilizowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao siku chache zilizopita wanajeshi wa utawala huo katili waliwashambulia kwa mabomu Waislamu waliokuwa wanasali ndani ya Msikiti huo.

Idara ya Wakfu ya mji wa Quds huko Palestina imeripoti kuwa, mapema leo asubuhi, maelfu ya Wapalestina wa mji wa Quds na viunga vyake wamemiminika kwenye Msikiti wa al Aqsa na kutekeleza ibada ya Sala ya Idul Fitr huku wakipiga takbiri kwa sauti kubwa na kuhinikiza eneo hilo takatifu.

Idara hiyo imesema pia kwamba wanajeshi wa Israel wamewazuia mamia ya Waislamu wa Palestina kufika kwenye Msikiti wa al Aqsa na walikuwa wanaruhusu watu wazima na wenye umri mkubwa tu kuvuka vizuizi vingi vilivyowekwa na wanajeshi hao.

Taarifa ya Idara ya Wakfu ya mji wa Quds huko Palestina imeongeza kuwa, licha ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kuweka vizuizi vingi vya kuwazuia Wapalestina kufika katika Msikiti wa al Aqsa na kuwazuia mamia ya Wapalestina hata wasiingie katika mji wa Quds, lakini maelfu ya Wapalestina wamefanikiwa kutekeleza ibada ya Sala ya Idul Fitr kwenye Msikiti huo.

Wapalestina waliofanikiwa kusali katika Msikiti wa al Aqsa wametangaza uungaji mkono wao kwa wenzao wanaodhulumiwa na kushambuliwa kikatili na Wazayuni hasa katika kitongoji cha Sheikh Jarrah na Ukanda wa Ghaza.

Ukatili wa wanajeshi wa Israel umeongezeka sana katika mwezi wa Ramadhani wa mwaka huu, na utawala wa Kizayuni umefanya jinai dhidi ya Waislamu wa Palestina na Kibla cha Kwanza cha Waislamu kiasi kwamba hata watu wasio Waislamu wanaendelea kulaani jinai hizo.

3971387

Kishikizo: quds sala idul fitr aqsa
captcha