IQNA

Kiongozi wa Hamas atoa wito kwa wapenda huru duniani kutetea Msikiti wa al Aqsa

19:47 - May 14, 2021
Habari ID: 3473908
TEHRAN (IQNA)- Mkuu wa Idara ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ameutaka Umma wa Kiislamu na Kiarabu kufanya maandamano na mikutano ya kutetea na kuunga mkono Msikiti wa al Aqsa na watu wa Palestina.

Wito huo wa Hamas umetolewa huku ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel zikiendelea kushambulia makazi ya raia wa Ukanda wa Gaza ambako zaidi ya raia 100 wameuawa hadi sasa.

Katika ujumbe wake huo wa leo ijumaa, Ismail Hania ameyataka mataifa yote ya Kiislamu na Kiarabu na watu huru kote duniani kufanya mikutano na maandamano ya kutetea Msikiti wa al Aqsa na watu wa Ukanda wa Gaza na kuliunga mkono taifa la Palestina linalopigania haki zake. 

Hania pia amelishukuru taifa la Palestina, mataifa ya Kiislamu na Kiarabu na watu wote huru duniani kwa kuendelea kusimama kidete mbele ya dhulma za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa siku ya tano mtawalia, jeshi la utawala haramu wa Israel limeendelea kushambulia kinyama watu wa Ukanda wa Gaza na kubomoa makazi ya raia, miundombinu na kuangamiza kizazi. 

Takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina zineonesha kuwa, raia 119 wa Palestina wameuawa shahidi katika mashambulizi hayo ya kinyama ya jeshi la Israel. 27 kati ya waliouawa ni watoto wadogo na 11 ni wanawake. Wapalestina wengine 600 wamejeruhiwa. 

Makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza yamejibu hujuma hiyo kwa kuvurumisha mamia ya makombora katika miji ya Israel ukiwemo mji wa Tel Aviv na kusababisha hasara kubwa. Waisraeli wasiopungua 9 wameangamizwa katika operesheni hizo za kulipiza kisasi za Wapalestina na wengine 130 wamejeruhiwa.    

3971477

captcha