IQNA

Sheikh Mkuu wa Al Azhar atuma ujumbe kwa lugha 15, ikiwemo Kiswahili, kuhusu Palestina

15:08 - May 16, 2021
Habari ID: 3473916
TEHRAN (IQNA)- Sheikh Mkuu wa Chuo cha Kiislamu cha Al Azhar nchini Misri ametuma ujumbe kwa lugha 15 akitaka dunia iwaunge mkono Wapalestina wanaokandamizwa na utawala haramu wa Israel.

Katika ujumbe wake alioutuma Ijumaa, Sheikh Ahmed el Tayyib ametoa wito kwa mataifa na viongozi wa dunia kuunga mkono watu taifa lipendalo amani la Palestina ambalo linadhulumiwa kwa sababu tu linatetea haki zake za kisheria kwa lengo ya kukomboa ardhi zake na maeneo yake matukufu yaliyoghusubiwa.

Aidha ametaka mauaji ya Wapalestina yasitishwe na warejeshewe ardhi zao. Halikadhalika ameitaka dunia ivunje kimya na iache sera za undumakuwuli iwapo kweli wote wanataka amani. Katika ujumbe huo uliokuwa kwa lugha ya Kiarabu na lugha zingine 14 zikiwemo Kifaransa, Kiingereza na Kiswahili, Sheikh el Tayyib amemuomba Mwenyezi Mungu awarehemu mashahidi wa Palestina na awapokee kwa rehma na maghfira.Sheikh Mkuu wa Al Azhar atuma ujumbe kwa lugha 15, ikiwemo Kiswahili, kuhusu Palestina

Tokea Jumatatu hadi leo Jumapili, Wapalestina 170, wakiwemo watoto 41, wameuawa shahidi katika  hujuma hii mpya ya utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Ghaza huku wengine 1,000 wakijeruhiwa.

Utawala ghasibu wa Israel ulianzisha uvamizi dhidi ya Ghaza baada ya Wapalestina katika eneo hilo kuandamana kulalamikia vikali ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina katika mji wa Quds (Jerusalem). Kitendo cha askari katili wa Israel kuuvamia Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds na kuwahujumu Wapalestina waliokuwa wakiswali katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kimehesabiwa kuwa ni kuvuka mstari mwekundu wa Wapalestina na Waislamu duniani.

Katika kujibu jinai hizo za Israel makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza yamevurumisha mamia ya makombora katika miji ya Israel ukiwemo mji mkuu Tel Aviv na kusababisha hasara kubwa. Wazayuni wasiopungua 10 wameangamizwa katika oparesheni hizo za ulipizaji kisasi za Wapalestina. 

3971562

 

captcha