IQNA

Netanyahu mtenda jinai atupwa katika jaa la taka za historia

19:52 - June 14, 2021
Habari ID: 3474006
TEHRAN (IQNA)- Benjamin Netanyahu mtenda jinai ametimuliwa madarakani na kufikia tamati utawala wake wa miaka 12 katika utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hii ni baada ya bunge la utawala huo haramu (Knesset) kupiga kura ya kuidhinisha serikali mpya ya muungano jana Jumapili na kwa msingi huo Netanyahu ametupwa katika jaa la taka za historia.

Kinara wa mrengo wa kulia wa chama cha Yamini (New Right), Naftali Bennett tayari ameapishwa kurithi mikoba ya Netanyahu, ambapo ataongoza kile kilichotajwa kuwa eti ni serikali ya mageuzi katika utawala huo bandia wa Israel.

 Bennett atakuwa Waziri Mkuu hadi mwezi Septemba 2023, na kisha atamkabidhi Yair Lapid, kiongozi wa chama cha mrengo wa kati cha Yesh Atid, kuongoza kwa miaka mingine miwili.

Waisraeli wamemiminika mabarabarani na mitaani kwa shangwe na vifijo kusherehekea hatua hiyo ya kutimuliwa madarakani Netanyahu, ambaye wamekuwa wakimtaja kama "Waziri wa Jinai."

Viongozi mbali mbali duniani, wakiwemo waitifaki wa utawala huo khabithi kama Rais wa Marekani Joe Biden na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel tayari wametuma salamu za pongezi kwa Bennett, wakisema kwamba wako tayari kufanya kazi naye.

Tangu mwezi Mei mwaka jana 2020, Netanyahu anapambana na kesi kadhaa za ufisadi, utapeli, kufilisi mali n.k, na sasa baada ya kutimuliwa madarakani, hana kinga yoyote ya kutoshitakiwa.

Bennett ambaye ana misimamo ya kuchupa mipaka ya mrengo wa kulia, amekuwa akitangaza wazi wazi misimamo yake hasi dhidi ya kuundwa taifa huru la Palestina; na kama Nentanyahu, ni mpinzani mkubwa pia wa makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya Iran.

Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif aliashiria mchakato wa kuondolewa Benjamin Netanyahu katika nafasi ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema, Netanyahu pia ametupwa katika jaa la taka za historia.

Katika ujumbe alioutuma katika ukurasa wake wa Twitter, Zarif ameashiria kufika ukingoni utawala wa Netanyahu na pia akamtaja rais wa zamani wa Marekani Donald Trump na maafisa wake wawili waliokuwa na misimamo ya kufurutu ada dhidi ya Iran ambao ni aliyekuwa mshauri wake wa usalama wa taifa John Bolton na aliyekuwa waziri wake wa mambo ya nje Mike Pompeo na kusema watatu hao walikuwa washirika wa Netanyahu katika misimamo yake dhidi ya Iran.

Zarif ameandika katika ukurasa huo wa Twitter kuwa: "Netanyahu amejiunga na wenzake waliuokuwa na misimamo mikali dhidi ya Iran yaani Bolton, Trump na Pompeo katika safari ya kuelekea katika jaa la taka za historia. Iran nayo inabaki ikiwa imesimama kidete na kwa heshima. Hii ndio hatima ya wale wote waliokuwa wakitaka kuidhuru Iran."

3977319

captcha