IQNA

Wanazuoni Iraq wakaribisha mapatano ya kuondoka askari wa Marekani nchini humo

22:24 - July 27, 2021
Habari ID: 3474131
TEHRAN (IQNA)- Mirengo miwili ya Al Fat-h na An-Nasr pamoja na harakati ya Hekima ya Kitaifa na ile ya Sadr nchini Iraq zimekaribisha juhudi za timu ya mazungumzo ya nchi hiyo zilizowezesha kufikiwa makubaliano na Marekani ya kuwaondoa askari wake katika ardhi ya Iraq.

Muungano wa Fat-h unaoongozwa na Hadi al A'merii umeeleza katika taarifa kwamba, juhudi za timu ya mazungumzo ya nchi hiyo iliyowezesha kufikiwa makubaliano na Marekani ya kuwaondoka askari wake katika ardhi ya Iraq ni hatua chanya katika kuhakikisha nchi hiyo inakuwa mamlaka yake kamili ya kujitawala; na imesema inatumai viongozi husika wa Iraq watafuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo.

Nao muungano wa An-Nasr unaoongozwa na Haidar al Abadi, umetoa taarifa pia na kusisitiza kuwa, matokeo ya mazungumzo kati ya Iraq na Marekani ni ushindi kwa maslahi na kujitawala kwa nchi hiyo na ukawatolea mwito Wairaq wote kuwa na mshikamano wa kitaifa katika masuala makubwa yanayoihusu nchi yao.

Wakati huohuo Ammar al Hakim, kiongozi wa harakati ya Hikma ya Kitaifa amesema, msimamo wa waziri mkuu na timu ya wawakilishi wa Iraq katika mazungumzo ya Washington umeleta mafanikio; na akaongeza kuwa, kwa uungaji mkono wa makundi ya kisiasa, timu hiyo ya wawakilishi wa Iraq imeweza kupata mafanikio ya kidiplomasia kwa kusaini makubaliano ya kuondoka kikamilifu askari wa Marekani nchini Iraq na kubakisha ushirikiano baina ya nchi mbili wa masuala ya utoaji mafunzo, ushauri na intelijensia tu.

Rais Joe Biden wa Marekani na Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa Al Kadhimi, siku ya Jumatatu walifikia makubaliano ya kuhitimisha rasmi uwepo wa miaka 18 kijeshi wa askari wa Marekani nchini Iraq ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2021.

Makubaliano hayo kati ya viongozi wa Marekani na Iraq yamefikiwa katika hali ambayo, kwa muda mrefu sasa wananchi na makundi mengi nchini Iraq yanataka askari wa jeshi la Marekani waondoke nchini humo, ikikumbukwa pia kuwa mnamo tarehe 5 Januari, 2020, bunge la Iraq lilipitisha mpango wa kutaka majeshi yote ya kigeni yaondoke katika ardhi ya nchi hiyo.

3986651

Kishikizo: iraq marekani ASKARI
captcha