IQNA

Ifahamu Siku Kuu ya Idul Ghadir

10:13 - July 29, 2021
Habari ID: 3474138
TEHRAN (IQNA)- Leo Alhamisi tarehe 29 Julai mwaka 2021 inayosadifiana na tarehe 18 Dhul-hija mwaka 1442 Hijria ni Sikukuu ya Idul Ghadir Khum, moja ya Idd kubwa za Waislamu.

Ghadir Khum ni eneo lililoko baina ya Makka na Madina ambako Mtume Muhammad (S.A.W) akiwa katika safari yake ya mwisho ya Hija  kwa amri ya Mwenyezi Mungu alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib AS kuwa kiongozi wa Waislamu wote baada yake. 

Katika makala hii tutajaribu kueleza kwa kifupi maana ya Siku Kuu ya Ghadir.

Idi kati ya mataifa ya dunia ni siku ya kuhuisha mila na desturi, kutangaza utiifu na kukumbuka siku muhimu mno za mataifa hayo. Baada ya Bwana Mtume Muhammad SAW kutekeleza ibada yake ya mwisho ya Hija, alimtangaza Imam Ali AS kuwa wasii na kiongozi wa Waislamu baada yake na tukio hilo ndilo linaloipa utukufu sikukuu ya Ghadir. Siku hiyo uso wa Bwana Mtume Muhammad SAW ulijaa bashasha na aliwataka Waislamu wampongeze kwa mnasaba wa siku hiyo. Baada ya hapo zilirindima sauti za Waislamu kumpongeza Bwana Mtume na vile vile kumpongeza Imam Ali AS. Tukio hilo limetungiwa kasida mbalimbali na tangu wakati huo hadi leo hii, huadhimishwa kila mwaka. Sisi nasi hapa kwa mara nyingine tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Bwana Mtume Mtukufu SAW, kwa Imam Ali AS na kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba wa sikukuu ya Ghadir tukinukuu miongozo ya Imam Ridha AS aliposema: "Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia tushikamane na utiifu kwa Ali AS.

Baraka za Ghadir

Tarehe 18 Mfunguo Tatu Dhulhijja ni siku ya kufaidika na kustafidi vilivyo na baraka za Ghadir. Katika siku kama hii, Imam Sadiq AS alikuwa akitoa pongezi kwa marafiki zake na akimuomba Mwenyezi Mungu awamiminie baraka zake waja Wake ambao wanaunga na Waislamu wenzao katika sikukuu ya Ghadir na kuzungumza nao kuhusu sira na mwenendo mtukufu wa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Idi maana yake ni kama kuzaliwa upya. Imam Hasan AS mmoja wa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa akifanya hafla kubwa mjini Kufa Iraq kila ilipokuwa ikiingia sikukuu ya Ghadir. Imam Hasan AS alikuwa akitoa zawadi nyingi kwa watu katika sikukuu ya Ghadir.Harakati ya uongofu na uongozi wa wanaadamu umegawanyika kwenye awamu mbili katika kipindi chote cha historia. Awamu ya kwanza inaanzia kwa Nabii Adam akiwa Mtume wa kwanza kabisa wa Mwenyezi Mungu na kufuatiwa Mitume na Manabii wengi baada yake hadi kufikia kwenye Mtume wa Mwisho, Bwana wetu Muhammad SAW.Amma awamu ya pili ya uongozi wa wanaadamu inaanzia mwezi 17 Mfunguo Tatu wakati Bwana Mtume Muhammad SAW alipomtangaza Imam Ali AS kuwa Kiongozi wa Waislamu baada yake. Katika sekunde hizo za kihistoria, Bwana Mtume alipokea amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya kuwatangaza viongozi wa baada yake ambapo kiongozi wa kwanza kabisa katika silisila hiyo alikuwa ni Imam Ali AS. Hapo ndipo ilipoanzia awamu ya pili ya uongozi wa wanaadamu. Baada ya tangazo hilo la Bwana Mtume SAW, Waislamu walimfuata Imam Ali AS na kumpongeza wakisema, "Hongera hongera ewe mwana wa Abu Talib, umekuwa kiongozi wetu na kiongozi wa wanaume na wanawake wote waumini."

Mkusanyiko eneo la Ghadir Khum

Ghadir ni siku ya kuzidi thamani ya shakhisa ya Ali AS. Mtukufu huyo aliyezaliwa ndani ya al Kaaba, alikuwa pamoja na Bwana Mtume SAW tangu awali ya kudhihiri Uislamu na kwenye mashaka na matatizo yote hadi alipopigwa upanga wa sumu akiwa amesujudu uliopelekea kuuawa shahidi. Ghadir ni siku ambayo Bwana Mtume Muhammad SAW aliwakusanya pamoja maelfu ya Waislamu ambapo baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa walifika Waislamu laki moja na 20 elfu ambao walikuwa wanarejea makwao kutoka katika amali tukufu ya Hija. Aliwakusanya kwenye eneo lenye joto kali la Ghadir Khum kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Sauti za misafara ya mahujaji na kengele za ngamia zilihinikiza angani. Bwana Mtume alizama kwenye mawazo mazito, alionekana anasubiri habari muhimu sana. Ghafla alishukiwa na wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Bwana Mtume akatoa amri kwamba wale ambao walikuwa hawajafika mahala hapo, waongeze mwendo ili wafike haraka na wale waliokuwa wameshatangulia mbele warejee.Mjumuiko mkubwa wa Waislamu ulikusanyika katika eneo hilo, huku baadhi ya wapokezi wanasema walikuwa ni watu elfu 90, wengine wanasema walikuwa ni laki moja na wengine wanasema Waislamu waliokusanyika hapo walikuwa ni laki moja na 20 elfu. Hali ya hewa wakati huo ilikuwa ya joto kali kiasi kwamba watu waliokuwa wakiishi Jaziratul Arab, ambao wengi wao ni wakazi wa majangwani waliozoea hali ya joto, wao pia walishindwa kuvumilia joto la sehemu hiyo. Ardhi ilikuwa inafuka moto na hivyo walilazimika kuvua majoho yao na kuyaweka chini ya miguu yao ili waweze kupunguza ukali wa joto hilo. Nukta hii imezungumziwa pia na wapokezi wa Kisuni.

Tangazo muhimu

Baadaye Bwana Mtume Muhammad SAW alisimama na kumtaka pia Amirul Muminin Ali AS asimame, halafu alisimama juu ya kijukwaa na kuunyanyua mkono wa Imam Ali AS akisema:

«من كنت مولاه فهذا على مولاه، اللهم وال من والاه و عاد من عاداه»

Mtu ambaye mimi ninamsimamia mambo yake, (yaani ambaye mimi ni kiongozi wake) basi na huyu Ali naye anamsimamia mambo yake. Mwenyezi Mungu kuwa pamoja na aliye pamoja na Ali na kuwa adui wa anayemfanyia uadui Ali. 

Tab'an maneno hayo yapo katikati ya maneno mengine yaliyotangulia na yaliyokuja baada ya matamshi hayo yaliyomo kwenye hotuba ndefu ya Bwana Mtume aliyoitoa siku hiyo. Hata hivyo sehemu hiyo ndiyo muhimu zaidi ambayo ndani yake Bwana Mtume Muhammad SAW alitangaza Wilaya - yaani utawala wa Kiislamu - kwa njia rasmi na ya wazi kabisa, na alimtangaza Amirul Muminin Ali AS kuwa mtu aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo. Hilo limezungumzwa pia kwa uwazi na ndugu zetu wa Kisuni katika vitabu vyao vinavyokubalika - wala si katika kitabu kimoja au viwili tu, bali katika makumi ya vitabu vinavyokubalika. Marhum Allama Amini amevijumuisha vitabu hivyo katika kitabu chake cha al Ghadir. Mbali na hivyo pia, kuna vitabu vingine mbalimbali kuhusu suala hilo. 

Umuhimu wa Sikukuu ya Ghadir Khum

Ni jambo lisilo na shaka kwamba sikukuu ya Ghadir ina umuhimu mkubwa. Umuhimu wa siku hiyo umepokewa katika hadithi mbalimbali za Kiislamu na tunaweza kusema hata zaidi ya hadithi zinazohusiana na Idul Fitr na Idul Adh-ha. Hii haina maana kwamba umuhimu wa idi hizo mbili kubwa za Kiislamu ni mdogo au umepungua, hapana, bali ni kwa sababu idi hii ya Ghadir inahusiana na kitu kimoja muhimu zaidi. Kwa mujibu wa Hadithi za Kiislamu kinachofanya Idul Ghadir kuwa na umuhimu mkubwa ni kwa kuwa inahusiana na suala la Wilaya yaani uongozi wa Kiislamu. Labda tunaweza kusema kuwa, lengo la kazi yote kubwa ya Mitume na watu wakubwa wa dini na Manabii wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani ziwaendee wote) ni huko kusimamisha Wilaya ya Mwenyezi Mungu. Ushahidi wa hayo umo katika Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Sadiq AS ambaye anasema kuhusu nafasi ya lengo la jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na jitihada nyinginezo katika dini kwamba lengo lake ni:

«ليخرج الناس من عبادة العبيد الى عبادت الله و من ولايت العبيد الى ولايت الله» 

Yaani: Watu waweze kutoka kutoka katika ibada ya kiumbe na waingie katika ibada ya Mwenyezi Mungu na watoke kwenye Wilaya na uongozi wa kiumbe na waingie chini ya Wilaya na uongozi wa Mwenyezi Mungu. 

Wilaya ya Mwenyezi Mungu

Naam lengo ni kuwa watu watoke chini ya udhibiti na uongozi wa viumbe kwa maana yake pana na halisi na waingie chini ya uongozi wa Mwenyezi Mungu tu. Amma katika sikukuu ya Ghadir kuna na nukta nyingine muhimu nayo ni kwamba kuna mawanda aina mbili katika suala la Wilaya; mosi ni uwanda wa nafsi ya mwanaadamu yaani mwanaadamu mwenyewe aweze - kwa msaada wa Mwenyezi Mungu - kuidhibiti na kuiweka chini ya Wilaya nafsi yake yaani kuiweka nafsi yake hiyo chini ya udhibiti na Wilaya ya Mwenyezi Mungu na uwanda wa pili ni kuwa aweze kuyaingiza mazingira ya maisha yake chini ya utawala na Wilaya ya Mwenyezi Mungu. Hii ina maana kuwa, jamii ya mwanaadamu inatakiwa iende kwa mujibu wa uongozi wa Mwenyezi Mungu. Kusiwe na Wilaya yoyote itakayoweza kuizuia jamii kuwa chini ya utawala na Wilaya ya Mwenyezi Mungu, si Wilaya ya fedha, si Wilaya ya kabila na kaumu fulani, si Wilaya ya kutumia mabavu, si Wilaya ya mila, desturi na ada ghalati bali utawala pekee uwe wa Mwenyezi Mungu. Mtu aliyetangazwa siku hiyo, ni mtu mtukufu, Imam Ali AS, walii wa wachaji Mungu ambaye ni kigezo bora cha kuigwa katika mawanda yote mawili ya Wilaya. Naam katika uwanda wa Wilaya ya nafsi binafsi ya mja na na suala zima la mtu kuidhibiti nafsi yake hiyo nao ndio huo uwanda wa kwanza wa Wilaya, na pia katika ruwaza na mfano aliouonyesha wa utawala wa Kiislamu wa Wilaya ya Mwenyezi Mungu katika miaka michache aliyotawala mtukufu huyo. Kigezo kilichoonyeshwa na mtukufu huyo kimebakia kuwa ruwaza njema hadi leo hii na kitaendelea kuwa hivyo katika historia kiasi kwamba mtu yeyote anayetaka kuijua vyema Wilaya ya Mwenyezi Mungu, anaweza kupata kigezo kilichokamilika kutoka kwa mtukufu huyo. 

Uongozi

Umuhimu wa kuwepo usimamiaji na uongozaji unaotakiwa suala la Ghadir na hatua ya Mtume Muhammad SAW ya kumtangaza Amirul Muminin Ali bin Abi Talib AS kuwa kiongozi wa kusimamia na kuendesha masuala ya uma wa Kiislamu ni tukio kubwa na lenye umuhimu wa aina yake katika suala zima la kuhusika moja kwa moja Mtume Muhammad SAW katika masuala ya uongozi wa jamii ya Kiislamu. Maana ya hatua hiyo iliyochukuliwa na bwana Mtume siku ya mwezi 18 Mfunguo Tatu Dhilhijjah mwaka wa 10 Hijria ni kwamba Uislamu unalipa umuhimu mkubwa suala la uongozi wa jamii. Kadhia ya Uongozi katika mfumo wa Kiislamu na katika jamii ya Kiislamu si kitu cha kuachiliwa vivi hivi kingie mikononi mwa mtu yeyote tu asiye na sifa zinazotakiwa. Na sababu yake ni kuwa uongozi wa jamii ni moja ya mambo yanayoacha athari kubwa sana katika jamii. Kuteuliwa Amirul Muminin Ali bin Abu Talib AS kubeba jukumu hilo na ambaye ni nembo ya ucha Mungu, elimu, ushujaa, kujitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu na uadilifu kati ya masahaba wa Bwana Mtume Muhammad SAW; kunazidi kuuweka wazi upeo mkubwa wa umuhimu wa jambo hilo. Uislamu hapo unatuwekea wazi kwamba sifa za kiongozi wa Kiislamu zinapaswa ziwe kama hizo alizojipamba nazo Imam Ali AS. Hata wale watu ambao hawakubali kwamba Imam Ali alikuwa wasii wa Bwana Mtume wa kuchukua uongozi mara baada ya kufariki dunia Mtume Muhammad SAW, nao hawana shaka hata chembe juu ya elimu, ucha Mungu, taqwa na ushujaa wa mtukufu huyo pamoja na kujitolea kwake katika njia ya Allah na katika kupigania haki na uadilifu. Waislamu wote wanaomtambua Amirul Muminin Ali bin Abi Talib AS wanakubaliana kwamba sifa hizo zilikuwa zimejikita katika shakhsia ya mtukufu huyo, Imam Ali AS.

Aidha hatua hiyo inaonyesha ni aina gani ya jamii ya Kiislamu inayotakiwa na Uislamu na Bwana Mtume na ni uongozi wa aina gani unaopaswa kufanywa kuwa ndilo lengo la kupiganiwa.

Uhakika Ulio Wazi na Uliojificha wa Ghadir

Kuna uhakika mwingi umejikita ndani ya tukio la Ghadir. Ukweli wa tukio hilo ni kwamba kazi iliyofanywa na Bwana Mtume Muhammad SAW kwa ajili ya jamii changa ya Kiislamu ya wakati huo ambayo iliundika katika kipindi cha miaka kumi hivi tangu ulipopata ushindi Uislamu, ilikuwa ni kutatua suala la serikali, uongozi na Uimamu kwa maana yake pana na ndio maana katika tukio la Ghadir Khum baada ya kutekeleza ibada yake ya mwisho ya Hijja na wakati alipokuwa anarejea Madina, aliwatangazia Waislamu mtu wa kushika nafasi yake, naye ni Amirul Muminin Ali bin Abi Talib AS. Hata hii dhahiri ya tukio hilo pekee ambayo tab'an ni muhimu sana, pia ina mazingatio makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya watu ambao wanayafanyia utafiti na kuyafuatilia masuala ya jamii ya kimapinduzi. Lakini pia kuna uhakika mwingine mkubwa umejificha ndani ya tukio hilo ambapo kama uma na jamii ya Kiislamu itaziangalia kwa kina nukta za uhakika huo, basi itafanikiwa kupata njia bora na ya wazi ya maisha. Kimsingi ni kwamba kama tukio la Ghadir litachukuliwa na Waislamu wote - wawe Waislamu wa Kishia ambao wanalijua vyema tukio hilo katika upande wake wa uongozi, uimamu na Wilaya, au Waislamu wengine ambao pamoja na kwamba wanakubali kuwa tukio hilo lililotokea lakini hawaliangalii kwa sura ya uongozi, uimamu na Wilaya - kama wote hao leo hii watazitilia maanani na kuzizingatia sana zile nukta muhimu zilizojikita katika tukio la Ghadir, basi wataweza kuwaletea mafanikio mengi Waislamu wote duniani. Miongoni mwa nukta hizo ni kwamba mosi huko kuteuliwa tu mtu mtukufu kama Imam Ali kuwa kiongozi wa Waislamu, pekee kuliweka wazi vigezo anavyopaswa kuwa navyo kiongozi wa Kiislamu.

Thamani za Kiislamu

Katika tukio hilo Mtume Muhammad SAW aliwateulia Waislamu mtu wa kuwaongoza ambaye alikuwa amekamilika katika sifa na thamani zote za Kiislamu. Alikuwa ni mtu muumini, aliyekuwa na kiwango cha juu kabisa cha taqwa na ucha Mungu, mwenye kujitolea katika njia ya Uislamu, ambaye hakuwa na tamaa hata chembe na mambo ya kidunia, aliyepata uzoefu na kushinda mitihani katika nyanja zote: nyanja hatari, nyanja za elimu na maarifa, nyanja za kutoa hukumu na kadha wa kadhalika. Yaani hatua ya Bwana Mtume SAW ya kumtangaza Amirul Muminin Ali AS kuwa kiongozi; awe Imam na walii wa Waislamu; kunawafunza Waislamu wote wa kipindi kizima cha historia kwamba mtawala wa Kiislamu lazima awe mtu ambaye atakuwa amepambika na sifa hizo hata kama hazitakuwa na ukamilifu kama aliokuwa nao Imam Ali AS. Maana ya maneno hayo ni kwamba mtu ambaye hana sifa hizo katika jamii za Kiislamu, ambaye hana welewa wa Uislamu, ambaye hatendi mambo yake kwa mujibu wa Uislamu na asiyezingatia jihadi, kutoa na kujitolea katika njia ya Uislamu, ambaye hana huruma wala unyenyekevu kwa waja wa Mwenyezi Mungu na ambaye hakujipamba kwa sifa yoyote katika sifa hizo za Amirul Muminin Imam Ali AS, mtu huyo hana haki ya kuongoza jamii za Kiislamu. Hilo ndilo alilotaka kutufunza Bwana Mtume na sifa na vigezo hivyo ndivyo ambavyo mtukufu huyo aliwabainishia Waislamu. Kwa kweli hilo ni somo lisiloweza kusahaulika. Nukta nyingine ambayo tunaweza kuipata katika tukio la Ghadir ni kuwa, Amirul Muminin Ali bin Abi Talib AS hata katika ile miaka michache aliyojaaliwa kutawala na kuongoza jamii ya Kiislamu, alionyesha kivitendo jambo linalopaswa kupewa kipaumbele na kiongozi wa nchi na jamii, nalo ni uadilifu wa Mwenyezi Mungu na wa Kiislamu. Yaani uadilifu; yaani kufanikisha lengo ambalo Qur'ani imelieleza kuwa ndiyo shabaha ya kutumwa Mitume na Manabii na kuteremshwa Vitabu na sheria za Mwenyezi Mungu. Qur'ani Tukufu inasema kuhusu jambo hilo kwamba:

لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ 

Ili wasimame watu katika uadilifu. al Hadidi (57:25) Yaani uadilifu wa Mwenyezi Mungu usimame.

Kwa hakika insafu na usawa kama ulivyoainishwa na Uislamu, ndiyo njia bora kabisa ya kudhamini na kuleta uadilifu na utangamano katika jamii. Kwa mtazamo wa Imam Ali bin Abi Talib AS, hilo ndilo jambo la kupewa kipaumbele cha kwanza katika uongozi. Maana ya Wilaya katika Tukio la GhadirKatika tukio la Ghadir, Bwana Mtume Muhammad SAW alitekeleza moja ya majukumu yake makubwa kwa mujibu wa amri ya Mwenyezi Mungu iliyokuja katika Qur'ani Tukufu kama aya inavyosema:

وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ 

...na kama hukufanya basi utakuwa hukufikisha ujumbe Wake. al Maida (5:67) 

Naam suala la kuteuliwa Amirul Muminin Ali AS kuwa walii na khalifa wa Waislamu lilikuwa muhimu kiasi kwamba kama Bwana Mtume asingelilifanya basi ingelikuwa ni sawa na kuwa hakufikisha risala na ujumbe aliotumwa na Mwenyezi Mungu kuufikisha! Yamkini makusudio ya aya hiyo ni kwamba atakuwa hakufikisha risala na ujumbe aliotumwa kuufikisha kuhusu amri hiyo yenyewe ya kumtangaza Imam Ali AS kuwa khalifa baada yake, kwani Mwenyezi Mungu amemuamrisha atekeleze wajibu huo. Aidha yamkini makusudio yakawa ni ya juu zaidi ya hivyo, kwa maana ya kwamba angelikuwa hakufikisha risala na ujumbe wote aliotumwa na Mwenyezi Mungu akiwa Mtume Wake kwa walimwengu, yaani kazi yote aliyotumwa ingeliingia dosari na doa kama asingelimtangaza Imam Ali AS kuwa kiongozi wa Waislamu baada yake. Uko uwezekano kwamba hiyo ndiyo maana ya maneno hayo ya Mwenyezi Mungu. Yaani ingelikuwa ni kana kwamba asili ya ujumbe wenyewe wa Utume haikufikishwa kwa walimwengu!

Na kama tutasema ni hivyo, basi umuhimu wa tukio la Ghadiri utakuwa mkubwa maradufu. Yaani suala la kuunda serikali, suala la Wilaya na utawala wa Kiislamu ni jambo ambalo limo katika matini asili ya dini na mafundisho ya Bwana Mtume Muhammad SAW na limepewa umuhimu mkubwa na tunaona jinsi Bwana Mtume alivyolitekeleza na kulifikisha mbele ya macho ya matabaka mbalimbali ya watu kwa hima na namna ambayo pengine hakuna wajibu wowote mwingine alioufikisha namna hiyo! Si Sala, si Zaka, si Funga na si Jihadi! Katika kuzifikisha kwa watu ibada na nguzo zote hizo za Mwenyezi Mungu, Bwana Mtume hakufanya kama alivyofanya katika upande wa Uimamu na utawala wa Waislamu. Yaani aliwakusanya watu wa matabaka tofauti, wa makabila mbalimbali na wa maeneo yote katika makutano ya njia za baina ya Makka na Madina kwa nia ya kufikisha amri hiyo ya Mwenyezi Mungu. Jambo hilo likaenea katika ulimwengu mzima wa Kiislamu.Maana ya Uimamu katika GhadirUimamu ni kilele cha maana inayotakiwa ya kuongoza jamii mbele ya anuwai kwa akisami za tawala za kibinaadamu zilizojaa udhaifu, hawaa za nafsi, ushaufu na kupenda jaha. Uislamu umemwonyesha mwanaadamu nuskha na namna ya Uimamu unavyopaswa kuwa. Yaani kiongozi inabidi awe mtu ambaye moyo wake umejaa baraka za uongofu wa Mwenyezi Mungu na awe na utambuzi kamili wa masuala ya dini. Yaani aweze kuainisha njia na kuongoza sirati vizuri, na awe na nguvu na uwezo mkubwa wa kiutendaji. Qur'ani Tukufu inasema:

يَا يَحْيَى خُذِ الْكِتَابَ بِقُوَّةٍ 

Ewe Yahya! Kishike Kitabu kwa nguvu... Surat Maryam (19:12) 

Aidha kiongozi anapaswa kuwa mtu ambaye hatajali zaidi nafsi yake, matakwa yake na maisha yake binafsi, bali roho, maisha na mafanikio ya wengine ndiyo yawe na umuhimu zaidi kwake. Jambo hilo lilionyeshwa kivitendo na Amirul Muminin Ali bin Abi Talib AS katika kipindi cha chini ya miaka mitano ya utawala wake. Naam, mnashuhudia wenyewe jinsi Imam Ali AS alivyofanikiwa katika kipindi kifupi cha chini ya miaka mitano kuunda na kuendesha serikali ambayo imekuwa ni kigezo na ruwaza bora isiyosahaulika kwa mwanaadamu na licha kupita karne nyingi tangu wakati huo, lakini hadi leo hii utawala huo umebakia hai na unang'ara mithili ya mbaamwezi. Hayo ndiyo matunda ya somo, maana na tafsili ya kweli ya tukio la Ghadir. Ghadir na Suala la Umoja wa Umma wa KiislamuKadhia ya Ghadir nayo inaweza kuwa chanzo cha kuleta umoja na mshikamano kati ya Waislamu. Yamkini mtu akaona kitu hicho ni cha ajabu na hakiwezekani, lakini huo ndio ukweli wenyewe. Suala lenyewe la Ghadir ukiachilia mbali ule upande ambao Waislamu wa Kishia wanauhesabu kuwa ni itikadi yao - yaani kuteuliwa Amirul Muminin Ali AS kuwa mtawala wa Waislamu baada ya Bwana Mtume Muhammad SAW kama inavyosema wazi hadithi ya Ghadir - kuna kitu kingine kinaonekana wazi katika tukio hilo nalo ni suala lenyewe la Wilaya na utawala wa Kiislamu. Suala hili la utawala wa Kiislamu halihusiani na Mashia au na Masuni peke yao. Kama leo Waislamu duniani, na kama mataifa yote ya Kiislamu yatashikamana katika kalima moja na iwapo wote watakuwa na kaulimbiu moja ya kusimamisha Wilaya na utawala wa Kiislamu, basi wataweza kufika mbali ambako hadi leo hawajafika, na watafanikiwa kuvuuka kwa fakhari vigingi vingi vinavyoukabili umma wa Kiislamu. Aidha watamudu kutatua matatizo mengi ya nchi za Kiislamu ambayo hadi leo yamekuwa vigumu kutatuka.

Kishikizo: ghadir khum idi
captcha