IQNA

Bendera ya Msikiti wa Jamkaran yabadilishwa kabla ya kuanza Muharram

TEHRAN (IQNA)- Katika mkesha wa kuanza mwezi wa Muharram, bendera ya Msikiti wa Jamkaran karibu na mji wa Qum nchini Iran imebadilishwa ambapo ile ya kijani kibichi imeshushwa na nyeusi ikapandishwa.

Kubadilisha bendera kunaashiria kuanza maombolezo  ya kukumbuka kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS.

Muharram ni mwezi wa kwanza wa mwaka wa Hijria Qamaria ambapo sasa tuko katika mwaka wa 1443.

Katika mwezi wa Muharram Waislamu, hasa wa madhehebu ya Shia, na wapenda haki kote duniani hukumbuka  tukio la Ashura ambalo lilijiri takribani miaka 1382 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Qamaria.

Katika tukio hilo, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya.

 
Kishikizo: muharram ، ashura ، jamkaran ، imam hussein