IQNA

Hamas yabainisha njama za kuanzishwa uhusiano na Israel

19:33 - September 19, 2021
Habari ID: 3474315
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kwa mara nyingine imelaani vikali mkataba wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya madola ya Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika taarifa Jumamosi, Hamas imesema  ‘Mkataba wa Abraham’ ambao ulitiwa saini baina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain ni hatari sana.

Maafikiano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya Israel na nchi mbili za Kiarabu za UAE na Bahrain yaliyojulikana kama makubaliano ya Abraham, yalitiwa saini tarehe 15 Septemba mwaka jana (2020) katika ikulu ya Marekani White House. 

Hamas imesema mapatano hayo yanalenga kuimarisha ukoloni wa kijeshi, kisiasa na kiuchumi wa Israel katika eneo sambamba na kupora utajiri wa eneo, kuitenga kadhia ya kupigania ukombozi wa Palestina na pia kuliteganisha taifa la Palestina na mataifa ya Kiarabu na Kiislamu duniani.

Hamas imeyataja mapatano hayo kuwa mpango wa Kizayuni-Marekani wenye lengo la kuibua  taharuki baina ya Waislamu kwa lengo la kuitenga kadhia ya kupigania ukombozi wa Palestina.

Mwaka 2020, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Morocco na Sudan ziliafiki  kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel kufuatia mashinikizo ya Marekani. Kitendo hicho kiliibua ghadhabu kote Palestina na kwingineko kote ulimwenguni wa Kiislamu ambapo hatua hiyo imetajwa kuwa ni usaliti mkubwa wa serikali za Kiarabu kwa malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina.

/3475738

captcha