IQNA

Mwanamke Muislamu Marekani alalamika kuvuliwa hijabu kituo cha polisi

23:16 - September 20, 2021
Habari ID: 3474319
TEHRAN (IQNA)- Mwanamke mmoja Muislamu katika jimbo la Michigan nchini Marekani amelalamika kuwa polisi walimvua Hijabu baada ya kumkamata. Alivuliwa Hijabu katika kituo cha polisi wakati wa kupigwa picha.

Bi.Helena Bowe, 40, (kwenye picha) anasema hajawahi kukamatwa maishani lakini Alhamisi alisimamishwa na polisi ambao walidai kuwa  alikuwa na bunduki ya mshtuko wa umeme ndani ya gari lake bila leseni. Kwa kawaida aina hii ya bunduki haina risasi na hutumiwa sana na wanawake Marekani kujikinga wanapovamiwa na wahalifu.

Akiwa katika kituo kimoja cha polisi mjini Ferndale, maafisa wa polisi walimlazimisha kuvua hijabu ili wampige picha ili kufungua faili la kesi yake.

Sasa Bowe anataka polisi wamlipie fidia ya dola 250,000 kwani kitendo hicho kilimsababishia msongo mkubwa wa mawazo.  Shirika la kutetea Waislamu Marekani lijulikanalo kama Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR), tawi la Michigan, kupitia wakili wake, Amy Doukoure limesema linafuatilia kesi hiyo.

Wakili Doukoure amesema tayari wameshawasilisha kesi wakitaka Polisi ya Ferndale ilipe fidia na iwaruhusu wanawake Waislamu wavae Hijabu kamili wanapopigwa picha.

Mkuu wa Polisi ya Ferndale Dennis Emmi amekiri kuwa Bowe alilazimishwa kuvua Hijabu na kudai kuwa walifanya hivyo kwa mujibu wa sheria. Hatahivyo amesema watawasiliana na CAIR kuona ni vipi wanaweza kuwahudumia Waislamu.

Bowe ambaye ni Muislamu Mmarekani mwenye asili ya Afrika anasema kilichomkasirisha zaidi ni kuwa alikamatwa na afisa mwanaume aliyemvunjia heshima na pia katika kituo alifanyiwa upekuzi na afisa mwanaume. Mambo hayo yalimzidishia zaidi msongo wa mawazo kwani haki zake kama Muislamu zilikiukwa kikamilifu. Halikadhalika anasema hivi karibuni majaji katika majimbo mawili Marekani walitoa hukumu na kusema ni haki ya mwanamke kuvaa Hijabu wakati anapopigwa picha katika idara za serikali. Aidha anasema alilazimika kutumia bunduki ya mshtuko wa umeme baada ya kuhujumiwa na wahalifu. Baadhi ya majimbo Marekani huruhusia aina hii ya bunduki kumilikiwa na raia hata bila leseni.

Bi. Bowe alibubujikwa na machozi wakati alipokuwa akisimulia mbele ya waandishi habari masaibu aliyopata mikononi mwa maafisa hao wa polisi ambao walionekana kuwa na chuki ya wazi dhidi ya Waislamu.

3998892/

captcha